Yanga yatabiri fainali ya kibabe FA

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 04:39 PM Jun 04 2025
Yanga yatabiri fainali ya kibabe FA
Picha: Mtandao
Yanga yatabiri fainali ya kibabe FA

Klabu ya Yanga imesema mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati yao dhidi ya Singida Black Stars itakuwa moja ya fainali ngumu na ya kibabe kuwahi kutokea kwenye michuano hiyo.

Yanga inatarajia kucheza na Singida Black Stars mchezo huo wa fainali kati ya Juni 26 na 28 mwaka huu ikiwa ni siku chache baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu.

Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema leo kuwa wameanza kujipanga na mchezo huo mgumu na wanafahamu ugumu watakaokutana nao mbele ya wapinzani wao hao.

"Mchezo dhidi ya Singida Black Stars utakuwa mchezo mgumu sana, mara zote msimu huu tuliokutana nao mchezo ulikuwa mgumu, tulipata ushindi lakini kwa shida mechi zote tumewafunga Singida kihalali  lakini tunapata ushindani mkubwa kutoka kwao," amesema Kamwe.

Aidha, amesema msimu huu Singida imekuwa na ubora mkubwa kushinda timu nyingi msimu huuna ndio sababu ya kufanikiwa kutinga hatua hiyo ya fainali.

"Mashabiki na wadau wa soka watarajie fainali ngumu na yenye uhusiano, kama ingeingia timu nyingine kuja kucheza na Yanga, basi fainali hiyo ingekuwa ya upande mmoja, Singida mshindani wa kweli," amesema.

Katika hatua nyingine, Kamwe, alisema mbali na mchezo huo wa fainali ya FA, Yanga imebakisha mechi mbili pekee kumaliza msimu huu kabla ya kujipanga kwa ajili yamsimu ujao  pamoja na mashindano ya kimataifa.

"Sisi tumebakisha michezo mitatu kumaliza msimu huu wa 2024/2025, tumebakisha michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji pamoja na fainali ya FA dhdi ya Singida Black Stars," amesema Kamwe kwa msisitizo.