Hongereni TFF kwa kuendelea kufungia viwanja vibovu Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:46 AM Mar 17 2025
Viwanja vibovu
Picha:Mtandao
Viwanja vibovu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF), safari hii halicheki na mtu. Limeendelea kuvifungia viwanja ambavyo linaona havikidhi vigezo kikanuni.

Mpaka sasa limefungia viwanja vinne, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kufungiwa kwa wakati mmoja kwenye historia ya soka la nchi hii.

Viwanja ambavyo vimepigwa kufuli ni Ali Hassan Mwinyi, unaotumiwa na Tabora United, Uwanja wa Liti, Singida, ambao hutumiwa na Singida Black Stars, CCM Kirumba, Mwanza ambao ni nyumbani kwa timu ya Pamba Jiji na Jamhuri Dodoma unaotumiwa na Dodoma Jiji.

Timu hizo sasa zimelazimika kusaka njia mbadala ya kusaka viwanja vingine kwa ajili ya kucheza michezo yao ya Ligi Kuu na Kombe la FA.

Kwanza kabisa ningependa kuipongeza TFF kwa kuendelea kusimamia msimamo wake ule ule ambao Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia, alilisema mwanzoni kabisa mwa msimu kuwa watakuwa wakali kwa viwanja ambavyo havitakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa ajili ya mchezo.

Alisema anataka kuhakikisha mpira unachezwa kwa hali inayoridhisha kwa wachezaji na watazamaji wanaokuwa uwanjani na wanaoangalia kwenye televisheni. Ukiangalia sana viwanja vingi vinavyofungiwa tatizo linakuwa ni eneo la kuchezea 'pitch'.

Ni mara chache sana kuona viwanja vya hapa nchini vinafungiwa kwa mapungufu kama majukwaa, uzio, vyoo, na miundombinu mingine zaidi ya eneo la kuchezea.

Nadhani hili ndilo tatizo kubwa kwenye viwanja vya Tanzania na sasa linaonekana kama linataka kuwa janga la kitaifa kwenye mchezo wa soka.

Kwangu binafsi naona kuna uzembe mkubwa kwa wamiliki wa viwanja, pamoja na mameneja na sababu zinazotolewa.

Nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa na mvua kwa kiasi cha angalau robo ya mwaka mzima. Ina mito, maziwa, mabwawa, yaani kwa kiasi kikubwa haina tatizo la maji.

Inakuwaje viwanja vinakuwa vikame, vikavu kiasi cha wakati mwingine uwanja unakuwa mgumu na mpira unadundadunda kama ardhi ambayo imechomwa moto na kuachwa?

Siku hizi kuna matanki mengi tu ya kuhifadhia maji, lakini pia kuna visima vya kuchimbwa, inakuwaje viwanja vikubwa kama hivi viwe na tatizo sehemu ya kuchezea?

Cha ajabu ni kwamba vinapofungiwa tu, papo hapo hatua za haraka huchukuliwa. Hata wiki haijaisha utaona pilikapilika ya kusawazisha udogo sawa uwanjani, maji ndiyo yanapatikana na viwanja kumwagiwa. Harakati hizi zote zinazoonekana wakati viwanja vinafungiwa kwa nini zisionekana kabla ili viwe katika hali nzuri wakati wote?

Hapa ndipo inaonesha kuwa kumbe uwezo upo, ila tatizo ni uzembe. Kwa maana hiyo naishauri TFF ishikilie uzi huo huo. Hata kama ligi itachezwa kwenye viwanja viwili sawa tu, lakini hatuwezi kukubali mechi kuchezwa kwenye viwanja ambavyo hata watu wanaoangalia kwenye televisheni na wamelipia ving'amuzi vyao, wanashangaa kama wanachoona ni Ligi Kuu, au mechi za mchangani.

Siwezi kumaliza kama sitowapongeza wasimamizi wa Viwanja vya Tanzania Kwaraa, Babati mkoani Manyara, Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam, na Azam Complex, Chamazi, ambao wanaonesha kuipenda kazi yao na kuviweka kwenye hali nzuri na bora wakati wote kwa watazamaji na wachezaji pia.