NARUDIA kauli aliyosema winga wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Simon Msuva kuwa wanakwenda kuwashangaza Wamorocco kwao.
Ukimwangalia Msuva alipokuwa akiongea maneno yake, uso wake na mwili vyote vilikuwa vimemaanisha alivyokuwa akisema.
"Mechi iliyo mbele yetu siyo nyepesi kama watu anavyoifikiria, tumeshacheza nao zaidi ya mara moja, tumepoteza zaidi ya mara moja pia, lakini kama wachezaji tunajiandaa, naamini huu mchezo tutafanya maajabu na watu hawatoamini," alisema.
Msuva, ndiye mchezaji mwenye wastani mzuri wa kufunga mabao mengi kwenye kikosi cha Stars kwenye muongo mmoja kwa sasa, hivyo anavyosema anamaanisha.
Stars itajitupa kwenye Uwanja wa Manispaa jijini Casablanca kucheza dhidi ya timu ya taifa ya Morocco katika mchezo wa raundi ya nne ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia, zinazotarajia kuchezwa kwenye nchi tatu za, Marekani, Mexico na Canada.
Kwa kujikumbusha tu ni kwamba Tanzania ipo kwenye Kundi E, ikiwa kwenye nafasi ya tatu ya msimamo na pointi zake sita.
Pointi hizo ilizopata kwa kushinda ugenini bao 1-0 dhidi ya Niger, Novemba 18, mwaka juzi, na ikashinda tena ugenini dhidi ya Zambia, Juni 11 mwaka jana.
Ilipoteza mchezo mmoja nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikifungwa mabao 2-0 dhidi ya Morocco, uliopigwa, Novemba 21, mwaka juzi.
Katika kundi hili, Morocco ndiyo inayoongoza ikishinda michezo yake yote mitatu, ikivuna pointi tisa, ambapo inahitaji tena pointi zingine tatu dhidi ya Stars ili ifikishe 12.
Stars inahitaji ushindi ili kufikisha tisa na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele kuwania tiketi hiyo.
Naungana na Msuva na wote wanaoitakia mema timu ya taifa ya Tanzania, wakiwa na matumaini ya kufanya vyema kwenye mchezo huo.
Licha ya kwamba kwenye mchezo wa kwanza, Stars ilichapwa mabao 2-0, lakini matumaini ya kushinda ugenini yapo kwa sababu rekodi za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Tanzania inashinda zaidi ikicheza ugenini kuliko nyumbani.
Ukiangalia hata kwenye michuano hii, mechi zote mbili ilizocheza ugenini dhidi ya Niger na Zambia ilipata ushindi wa bao 1-0.
Kwa maana hiyo inaweza kupigana kufa na kupona kuweza kushinda au walau kupata sare.
Soka la Afrika kwa sasa limebadilika sana, tunaona nchi nyingi ambazo awali hazikuwa maarufu sana kwenye soka, zikizifunga, au kuvitetemesha vigogo vya soka Afrika kwa miaka ya hivi karibuni.
Mfano mdogo, nchi kama Comoro ambayo miaka 10 tu iliyopita ilikuwa moja kati ya timu vibonde, hivi sasa ni moja kati ya nchi tishio kwenye soka Afrika.
Tanzania nayo ni hivyo hivyo, imekuwa moja kati timu isiyotabirika, yenye uwezo wa kupata matokeo yoyote kwenye uwanja wowote Afrika.
Rejea, Septemba 7, 2023, ilipokwenda kulazimisha suluhu ugenini dhidi ya Algeria iliyokuwa na wachezaji wengi waliocheza soka la kulipwa Ulaya, na kufanikiwa kutinga fainali za AFCON zilizopita.
Kama iliweza kulazimisha suluhu ugenini, basi inaweza pia kushinda au kulazimisha sare pia ugenini dhidi ya Morocco.
Ni kwa sababu timu hizi za Afrika Kaskazini, Algeria, Morocco, Tunisia, Misri, ni vigogo wa soka Afrika na zina mzani sawa.
Kama Stars iliivimbia Algeria kwao, kwa nini isiwe Morocco? Ni lazima tuwashangaze. Naitakia kila la heri Stars kesho kutwa pale Casablanca itakapokuwa inapeperusha bendera ya Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED