Tunahitaji elimu zaidi ya tulikofika, katika kujiandikisha kupiga kura

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:52 AM Mar 25 2025
   Tunahitaji elimu zaidi ya tulikofika,  katika kujiandikisha kupiga kura.
Picha:INEC
Tunahitaji elimu zaidi ya tulikofika, katika kujiandikisha kupiga kura.

UBORESHAJI Daftari la Kudumu la Wapigakura mkoani Dar es Salaam, linatarajiwa kumalizika leo, baada ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kuongeza siku mbili zaidi za uboreshaji wa daftari hilo.

 Sababu ya tume hiyo kuongeza siku zaidi, zilielezwa na mwenyekiti wake Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, ni kutokana na mwitikio mkubwa wa kujiandikisha kwa wakazi wa mkoa huo.
 
 Hata hivyo, kunayaliyojitokeza kwenye baadhi ya maeneo, wakati wa kuhamasisha wananchi kujiandikisha, ambayo yanaonyesha kuwa elimu ya mpigakura bado inahitajika.
 
 Hapa kuna kisa na mkasa kinaelezewa na mhamasishaji  kutoka taasisi binafsi, Selemani Bishangazi, aliyekuwa akizunguka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zao katika daftari hilo.
 
 Wakati akitoa elimu eneo la Gongo la Mboto Stendi, alkalizwa na maswali mbalimbali yakiwamo kwamba, kujiandikisha kuna faida gan? Ni hali inayoonyesha wapo baadhi ya watu wasiojua umuhimu wa kujiandikisha na kupewa kitambulisho cha mpigakura.
 
 Kwa mujibu wa Bishagazi, wapo wanaosema wanakwenda kujiandikisha wapate vitambulisho wavitumie kukopa simu katika maeneo yanayokopesha vifaa hivyo vya mawasiliano.
 
 Mbali na hao, ni kwamba wengine wanaambiwa kuwa wakiwa na vitambulisho vya aina hiyo ni rahisi kukopa mtandaoni.  

Lakini, wapo waliodai kuwa hawawezi kwenda kupiga kura kuchagua viongozi wanaokwenda kunufaika na familia zao.
 
 Kwa maelezo hayo, ni wazi kwamba elimu kuhusu matumizi sahihi ya vitambulisho vya mpigakura inapaswa kutolewa kwa wingi katika maeneo mbalimbali ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha.
 
 Dar es Salaam inayoaminika kwamba ina watu wengi waelewa, bado wapo wenye mawazo ya aina hiyo. Je, vijijini kukoje? Kwa nini watu wanaamini kwamba anayechaguliwa anakwenda kufaidi na familia yake?
 
 Lakini, ni kwanini vitambulisho visitumike kupigia kura badala yake viwe kwa kukopea fedha?  Hapa inawezekana kuna jambo la halijakaa sawa, hasa ukosefu wa elimu kuhusu matumizi ya vitambulisho hivyo.
 
 Vilevile, wanaochaguliwa kuongoza wananchi, ni vyema watimize majukumu yao ipasavyo ili kuwafanya wawe na imani nao badala ya kuonekana kama wanajinufaisha badala ya kutumikia umma.
 
 Ninaamini kwamba tume kwa kushirikiana na wadau wa uchaguzi, inaendelea kutoa elimu ya mpigakura, lakini si vibaya kasi ya utoaji elimu hiyo ikawa kubwa kufikia watu wengi zaidi.
 
 Kwa mujibu wa tume hiyo, ni kwamba iliamua kuongeza siku za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kutokana na mwitikio mkubwa wa watu waliojitokeza kuboresha na kujiandikisha.
 
 Lakini wingi huo usije ukawa ni kutaka vitambulisho ili wakafanyie mambo mengine, badala ya lengo lililokusudiwa na kushiriki katika uchaguzi ili kupata viongozi watakaoongozwa kwa miaka mitano ijayo.
 
 Kushiriki uchaguzi ni haki ya kila Mtanzania mwenye sifa zinazotakiwa ukiwamo kuwa raia wa kuzaliwa, kwani ndio njia sahihi kupata viongozi watakaosaidia kuleta maendeleo ya nchi.
 
 Ikumbukwe kuwa, uchaguzi unatoa nafasi kwa jamii kushirikiana kwa malengo ya pamoja, kwa sababu wanapojitokeza kushiriki uchaguzi, wanajenga mshikamano na kuimarisha sauti yao kama wananchi wenye dhamira ya kuona maendeleo na ustawi wao.
 
 Tume imekamilisha mizunguko 12 ya uboreshaji wa daftari hilo  katika mikoa 30 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tangu ilipozindua uboreshaji huo mkoani Kigoma Julai 20 mwaka jana.
 
 Inaelezwa na tume kuwa Dar es Salaam ni mkoa wa 31 katika mzunguko wa 13. Elimu ya mpigakura isaidie kupunguza mtazamo unakwenda kinyume na matumizi sahihi ya vitambulisho hivyo.