Utoro kidato cha kwanza ni bomu la baadaye, lidhibitiwe

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 11:46 AM Mar 20 2025
Nyundo ya Mahakama.
Picha: Mtandao
Nyundo ya Mahakama.

WANAFUNZI 46,671 walipangiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari mkoani Mara, kwa mwaka huu wa 2025, lakini hadi sasa inatajwa asilimia 17.7 ya wanafunzi hao hawajaripoti shuleni.


Kuna sababu mbalimbali zinazotajwa kuwapo kwa utoro huo, mojawapo ikiwa ni baadhi ya wanafunzi hao kukimbilia nchi jirani kwa lengo la kujishughulisha na ajira za utotoni na wengine kuzuiwa na wazazi na walezi wao ili wafanye shughuli za nyumbani badala ya kusoma.  
 
 Maelezo hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huo, Kanali Evansi Mtambi wakati akifungua kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Mkoa (RCC) mjini Musoma hivi karibuni.
 
 Taarifa ya utoro huo inamfanya mkuu huyo wa mkoa kuwaagiza wakuu wote wa wilaya mkoani mwake kuanza msako wa kuwanasa wanafunzi wote ambao hawajaripoti shuleni.
 
 Utoro huo ni kwa eneo moja tu la nchi, ninadhani ufuatiliaji ukifanyika kila mkoa, inawezekana kuna wanafunzi wengi wa kidato cha kwanza ambao bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa.
 
 Hata hivyo, utaratibu wa kumaliza tatizo hilo umekuwa ni ule ule wa msako kila mwaka, lakini badi utoro umeendelea kujitokeza kana kwamba hakuna lolote linalofanyika kudhibiti.
 
 Ninadhani umefika wakati sasa wa kubadili mbinu za kupambana na utoro huo ili ikiwezekana, kuwe na matokeo chanya, kwani vinginevyo huenda wanafunzi wengi zaidi wakaendelea kuwa watoro.
 
 Wazazi, walezi hawana budi kushirikiana na walimu kwa ajili ya kuimarisha nidhamu ya wanafunzi na kudhibiti utoro shuleni, pia, viongozi wa serikali za vijiji nao washirikishwe kikamilifu.
 
 Sio vibaya kama watakuwa na takwimu kamili za wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu elimu ya msingi na hata wale wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ili kupata idadi yao.
 
 Katika mazingira hayo, utoro unaweza kudhibitiwa, kwani itakuwa ni  rahisi kuwatambua, hivyo kama watakuwa wapo nyumbani wakati shule zimefunguliwa, itabidi wazazi na walezi wahojiwe.
 
 Mtindo wa msako kila mwaka umeonekana kama hauzai matunda kutokana na kuendelea kuwapo kwa utoro huo, hivyo si vibaya kuja na mbinu mpya ya kudhibiti mtindo huo hatari kwenye elimu.
 
 Ikumbukwe kuwa utoro unaharibu malengo baadaye ya wanafunzi katika elimu, hivyo ni vyema wazazi na walezi watimize wajibu wao wa kuwasomesha watoto badala ya kuruhusu wawe watoro.
 
 Kwa kawaida wanafunzi wanatakiwa kuwahi shuleni baada ya mwaka wa masomo kuanza, lakini kitendo cha baadhi yao kutoenda shule kwa sababu zisizo na mashiko hakifai.
 
  Inawezekana wapo ambao hushindwa kuhudhuria masomo kwa matatizo ya kiafya au wengine kuhamishiwa shuleni nyingine. Yote hayo ni sawa, lakini inapendeza kama wazazi na walezi wanatoa taarifa.
  
 Kutoa taarifa kunasaidia serikali kujua wanafunzi wangapi ni watoro, na wangapi wenye changamoto au waliohamishwa kwenda shule nyingine kuliko kukaa kimya na kuonekana kama watoro.
 
 Mtindo huu wa utoro usiwe ni jambo la kawaida miongoni mwa jamii, badala yake kila mmoja wetu ajihusishe kuudhibiti iwe ni kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali au kwa namna yoyote ile ya kuudhibiti.
 
 Wakati mwingine inashangaza kuona mwanafunzi amesoma miaka saba elimu ya msingi, lakini kuingia sekondari anagoma au kuzuiwa kana kwamba huo ndio mwisho wa elimu.
 
 Yawezekana adhabu inayotolewa kwa wazazi au walezi wasiopeleka watoto wao shule ni ndogo ndio maana utoro umeendelea kuwapo, kama ndivyo, basi nadhani ipo haja kuongeza adhabu ili mtindo huo uishe.
 
 Kwa nini baadhi ya wazazi na walezi wako tayari kuona watoto wakiwa nyumbani bila kuwahimiza kwenda shule? Kila mmoja wetu atafakari kisha achukue hatua za kuhakikisha mtoto wake anasoma.
 
 Ni aibu mtoto kuhitimu elimu ya msingi na kuachana kuendelea na elimu ya sekondari kwa  kufanya kazi ndogo au shughuliza nyumbani kuwasaidia wazazi wake. Wanafunzi waachwe wasome.