Vilio wazabuni kulipwa vifikiriwe, cha TPA Tanga sasa ni salamu tu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:33 AM Mar 11 2025
Bandari ya Tanga.
Picha: Mtandao
Bandari ya Tanga.

HUDUMA za kijamii hutegemewa na wananchi kwa kiwango kikubwa, ikiwamo barabara ambazo zikiwa bora na zinazopitika hurahisisha mchakato wa mawasiliano.

Ujenzi wa miundombinu ni ya ushirikiano, kati ya serikali na wazabuni ambao hupewa zabuni kukamilisha malengo ya serikali, kufanikisha maendeleo kwa jamii.

Sasa kuna kilio cha wazabuni wanaotoa huduma kwenye maeneo, tukisikia katika Bandari ya Tanga wiki hii, wakilalamika kucheleweshewa malipo yao, kwa zaidi ya miezi minne, kunasababisha watoa huduma hao kuathirika moja kwa moja na kutishia kufilisika.

Wazabuni hao kupitia chombo hiki cha habari, wanafikisha ujumbe wao, kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, baadhi yao wakisema miongoni mwao wapo wanaodai Sh. milioni 50 hadi Sh. milioni 400.

Wanasema madai hayo, wamewasilisha madai yao kwenye Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), mara kadhaa kwa ahadi ya kulipwa ndani ya wiki husika bila mafanikio.

Pia, wazabuni wanasema mikataba yao pamoja na bandari yanaonesha malipo yatafanyika ndani ya siku 30, baada ya sisi kutoa huduma, sasa ni takribani miezi minne.

Kutokana na hilo ni wazi watoa huduma hao wanaathirika moja kwa moja pamoja na mzunguko mzima wa kiuchumia kwa walioko chini yao, kwamba wapo watoa huduma wengine ambao hutegemea mnyororo wa wazabuni hao.

Wapo watoa huduma kama ya chakula hata mamalishe ambao huwa sehemu ya mradi huo ingawa si moja kwa moja, watakosa fedha za kuendesha shughuli zao kutokana na wanaowategemea kutolipwa kwa wakati.

Pia, wazabuni hao nao hukopa mitaji kutoka vyanzo tofauti vya kifedha ili kukamilisha miradi, hasa taasisi za kifedha na kadri wanavyochelewa kulipa, riba inazidi kuongezeka kila siku na hawana namna na huweza kufilisiwa.

Kwa mujibu wa wazabuni hao, baadhi yao wametoa huduma ya kupeleka vifaa vya ofisi (stationary), vifaa vya ujenzi, spea za magari na mitambo.

Februari 16 mwaka huu, Bunge lilipitisha ongezeko la Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2024/25 kwa Sh. bilioni 945.7 na kufikia Sh. trilioni 50.29 kutoka bajeti ya Sh. trilioni 49.34 iliyoidhinishwa awali.

Kati ya fedha hizo za nyongeza, Sh. bilioni 325.9 zitatumika kulipa malipo ya madeni ya watumishi, makandarasi na wazabuni wa ndani na ujenzi wa miundombinu ya serikali katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Licha ya kupitishwa fungu hilo la nyongeza, baadhi ya wazabuni hawajalipwa, hata kufunga safari hadi ofisi za Nipashe kupaza sauti.

Ni vyema watoa huduma hao wakalipwa kwa wakati ili kutimiza mahitaji yao ya kujikimu na kubaki katika shughuli zao, kwa manufaa yao na taifa vilevile.