BoT: Riba ya asilimia 6 kuendelea

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:15 PM Apr 05 2025
Naibu Gavana wa BoT, Dk. Yamungu Kayandabila
Picha: Mtandao
Naibu Gavana wa BoT, Dk. Yamungu Kayandabila

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6 kwa robo ya pili ya mwaka 2025.

Akizungumza jana Aprili 4,2025 Naibu Gavana wa BoT, Dk. Yamungu Kayandabila, alitangaza uamuzi huo kufuatia kikao cha kamati kilichofanyika Aprili 3, 2025.

"Uamuzi huu wa kamati unalenga kuukinga uchumi dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani," amesema Dk. Kayandabila.

Aidha, ameeleza kuwa BoT itaendelea kutekeleza sera ya fedha, ili kuhakikisha mfumuko wa bei na kasi ya ukuaji wa uchumi nchini vinabaki ndani ya malengo na riba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 4-8. 

Kuhusu mwenendo wa uchumi nchini, Kamati ya Sera ya Fedha imesema ripoti za utafiti kuhusu mtazamo wa soko, maoni ya wakuu wa kampuni mbalimbali nchini pamoja na tathmini iliyofanywa na kampuni ya Moodys mwezi Machi 2025, Tanzania ilibakizwa katika Daraja B1 ikiwa na mwelekeo imara.

Aidha, mazingira ya uchumi duniani katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 yaliimarika, ambapo shughuli za kiuchumi katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi ziliendelea kuimarika.

”Mwenendo huu unatarajiwa kuendelea katika robo zijazo za mwaka 2025.Hata hivyo, matarajio hayo mazuri ya uchumi yanaweza kuathiriwa endapo vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani itaongezeka,”amesema.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Benki Tanzania (TBA), Theobald Sabi, ameipongeza BoT na serikali kwa ujumla kwa kuendelea kusimamia vizuri uchumi wa nchi na ameishukuru BoT kwa ushirikiano mzuri kwa mabenki nchini ambao una mchango katika ustawi wa sekta ya fedha nchini.