Viwanda vya uzalishaji bidhaa za ngozi nchini vinatarajia kushiriki katika maonyesho ya Kimataifa ya Mtindo na Ubunifu ya Afrika (ASFW) jijini Nairobi, yanayotarajia kuanza kesho hadi Aprili 26, mwaka huu.
Maonyesho hayo pia yatajumuisha viwanda 17 vya kuzalisha bidhaa hizo hususani viatu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Sudani Kusini.
Viwanda hivyo ni Himo Tanners na Fay Fashion, kwamba ushiriki wao unatoa fursa kubwa kwa maendeleo ya biashara na kujitangaza kimataifa katika sekta ya viwanda.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Ofisa Mawasiliano kwa Umma kutoka Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC), Waqas Rafique, alisema hatua hiyo inaonyesha mafanikio ya Mpango wa Uboreshaji wa Ufikiaji wa Masoko kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaofadhiliwa na EU—ujulikanao kama MARKUP II.
Alisema mpango huo unatekelezwa na ITC kwa ushirikiano na Sekretarieti ya EAC na wadau wa kitaifa.
Rafique alisema: “Kama sehemu ya juhudi zake pana, MARKUP II pia inaunga mkono uzinduzi wa tuzo za ubora za Kanda ya EAC za mwaka 2025.
Alisema katika maonyesho yaliyofanyika mwaka jana kampuni tatu kutoka Tanzania—CAPS Limited, Kampuni ya Said Salim Bakhresa Ltd na Kilombero Sugar Ltd. (Bwana Sukari)—ziliibuka washindi katika makundi mbalimbali.
Rafique alisema Tanzania, ambayo ni mzalishaji wa pili kwa ukubwa wa mifugo barani Afrika, kwa sasa inasafirisha zaidi ngozi ghafi na bidhaa za ngozi zenye thamani ndogo.
Hivyo alisema MARKUP II inalenga kubadilisha hali hiyo kwa kuhimiza ongezeko la thamani, kuboresha upatikanaji wa masoko na kuimarisha uwezo wa biashara ndogo na za kati (MSMEs) katika sekta muhimu—ikiwamo ngozi, parachichi, kahawa, ufungaji na viungo.
Rafique alieleza kuwa kampuni hizo mbili za kitanzania zitaungana na zingine za kikanda zilizopo katika mnyororo wa thamani wa viatu vya ngozi na mapambo.
Alisema mpango huo unahusisha Tanzania Bara na Zanzibar, kwa kuzingatia zaidi kuboresha ushindani wa MSMEs katika minyororo ya thamani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED