TAASISI ya The African Leadership Initiative for Impact (ALII) kwa kushirikiana na HakiElimu imezindua mpango maalum uitwao: Tanzania NextGen Leaders Fellowship (TNLF) unaolenga kulea vipaji vya uongozi miongoni mwa wahitimu wa shule za sekondari ili kuwaandaa kuwa viongozi mahiri wa sasa na baadaye.
Joseph Malekela, Mkurugenzi wa Shirika la ALII, alielezea kuhusu programu hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa maombi ya kushiriki kwenye mpango huo.
Malekela alisema mpango huo uliopangwa kufanyika kila mwaka unatarajiwa kushirikisha washiriki 350 wenye umri wa miaka 17 hadi 19 kutoka mikoa 34 nchini, watakaopatiwa mafunzo ya uongozi na kuwezeshwa kwa njia ya elimu ya juu na baadaye kuunganishwa na waajiri kwa ajili ya mafunzo ya awali ya ajira pamoja na fursa za kazi na uongozi kulingana na ujuzi wao.
“Tanzania NextGen Leaders Fellowship imekusudiwa kutumia uwezo mkubwa wa vijana wa kidato cha sita ambao haujatumika kikamilifu, kwa kuwawezesha kuwa chachu ya ubunifu, ukuaji wa uchumi, na maendeleo endelevu. Aidha, inalenga kuwapa kizazi kijacho cha viongozi wa Tanzania zana, maarifa na mitandao muhimu ya kukabiliana na changamoto za ndani na kimataifa,” alisema.
Malekela aliongeza: “Utekelezaji wa programu hii unatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 13 hadi 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambapo utafanyika kwa awamu ili kuruhusu vijana hao kushiriki hatua nyingine muhimu za maendeleo yao kama mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.”
Kwa mujibu wake, maombi yote yatapokelewa kupitia barua pepe rasmi: info@alii-africa.or.tz kabla ya Mei 30 mwaka huu, ambapo nafasi itatolewa kwa mwanafunzi mmoja kutoka kila shule na si zaidi ya washiriki kumi kwa kila mkoa.
Alisisitiza masharti manne ya msingi kwa waombaji ambayo ni: kuwa Mtanzania mwenye umri kati ya miaka 17 hadi 19 (aliyezaliwa kati ya mwaka 2006 hadi 2008), awe msichana au mvulana aliyehitimu mwaka huu, atambuliwe kama kiongozi bora wa mwaka na awe na uwezo mzuri wa kuwasiliana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Kwa upande wake, Benedicta Mrema, Afisa Mpango wa Idara ya Ushirikishwaji wa Vyombo vya Habari na Utetezi kutoka HakiElimu, akinukuu takwimu za Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), alisema asilimia 48.8 ya wanawake walioajiriwa wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi. Hali inaashiria kuwa karibu nusu ya wanawake walioajiriwa hawana usalama wa ajira wala mafao.
“Mpango huu wa kipekee utasaidia kuziba pengo la kijinsia kwa kuwapatia wasichana ujuzi wa uongozi, ushauri wa kitaaluma, na mitandao ya kitaalamu. Kwa kuwaandaa kwa ajira rasmi na kuwaunganisha na fursa halisi, mpango huu unapunguza hatari ya wao kuingia kwenye sekta isiyo rasmi na kuwawezesha kustawi katika nafasi za uongozi na taaluma endelevu,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED