Mbunge mteule awasilisha kero ukosefu wa maji kwa Dk. Nchimbi

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 05:01 PM Sep 03 2025
Mbunge mteule awasilisha kero ukosefu wa maji kwa Dk. Nchimbi
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbunge mteule awasilisha kero ukosefu wa maji kwa Dk. Nchimbi

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Meatu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salum Khamis, amewasilisha kero ya ukosefu wa majisafi na salama kwa Mgombea Mwenza wa Urais, Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi, akiomba itatuliwe haraka.

Aliwasilisha kero hiyo leo Septemba 3, katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi ulioongozwa na Dk. Emmanuel Nchimbi, ambapo pamoja na mambo mengine Salum amemwomba kiongozi huyo kufikisha ombi hilo kwa Mgombea Urais, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Salum amesema kuwa Meatu ndilo jimbo lenye changamoto kubwa zaidi ya maji katika Mkoa wa Simiyu ukilinganisha na majimbo mengine.

Amefafanua kuwa, ingawa Ilani ya Uchaguzi ya CCM imepanga kulipatia suluhisho katika awamu ya pili, wanaiomba Serikali iwajumuishe kwenye awamu ya kwanza ili kupata ufumbuzi wa haraka.

Aidha, amebainisha kuwa wananchi wa Meatu wameendelea kukabiliana na tatizo hilo kwa kuchimba visima vidogo na kufunga pampu za maji, hatua inayowasaidia kupata maji ya matumizi hasa katika kipindi hiki cha ukosefu wa mvua.