BEI za jumla za mchele, mahindi na maharage zimeongezeka katika kipindi cha kuanzia Februari 2024 hadi Februari 2025, ripoti iliyotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inabainisha.
Akizungumzia mfumuko huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Haji Semboja, ametaja chanzo cha bei ya mazao hayo kupaa kuwa ni nguvu kazi ya uzalishaji maeneo ya vijijini kupungua baada ya vijana wengi kuhamia mijini.
"Watu wengi wanahamia mijini wakidhani kwamba kuna fursa nyingi, badala ya kubaki vijijini kujikita na kilimo, ambacho kimekuwa ni fursa ya kujikwamua kiuchumi," amesema Prof. Semboja.
Ametaja mabadiliko ya tabianchi ni changamoto nyingine inayochangia kupungua kwa uzalishaji mazao na kwamba kilimo kinahitaji kuwekewa mikakati ya kisasa, akiwahamasisha wakulima kutumia zana za kisasa ili kuongeza mavuno.
Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Kilimo, katika kipindi cha kuanzia Machi 24 hadi 28 mwaka huu, bei ya wastani wa kitaifa kwa kilo katika mazao ya mchele ni Sh. 2,300, mahindi Sh. 900 na maharage 2,700.
Katika Jiji la Dar es Saalam, bei ya mchele Kwa wastani unauzwa Sh. 3,000 kwa kilo, mahindi Sh. 1,100 na maharage Sh. 3,700.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED