Mfumo wa eMrejesho V2 kuwania tuzo za kidunia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:53 AM Apr 23 2025
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA),Subira Kaswaga.
Picha: Mtandao
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA),Subira Kaswaga.

Mfumo wa eMrejesho toleo la pili (eMrejeshoV2) kutoka Tanzania, umechaguliwa kuwania Tuzo za Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya TEHAMA mwaka 2025 (WSIS 2025).

Tuzo hizo hutolewa na WSIS, kwa uratibu wa Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (ITU), kwa lengo la kutambua na kuchochea miradi bunifu, inayotumia TEHAMA katika kuchangia maendeleo endelevu duniani.

Mfumo  wa eMrejesho  toleo la pili (V2), umechaguliwa katika kipengele cha Serikali Mtandao (e-Government AL C7),  ikiwa ni miongoni mwa mifumo 360 ya TEHAMA iliyofuzu hatua ya mchujo kutoka kwa zaidi ya maombi 1000 ya mifumo ya kidijitali yaliyowasilishwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Ikumbukwe kwamba, mfumo wa e-Mrejesho toleo la kwanza ulishinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Ubunifu katika Huduma za Umma kwa mwaka 2024 ‘UN Public Service Innovation Awards’ .

Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA),Subira Kaswaga amesema, e-GA ilipokea taarifa ya ushiriki wa tuzo hizo hivi karibuni kupitia baruapepe kutoka ITU, baada ya mfumo wa e-Mrejesho kuchaguliwa kuwania tuzo hizo.

Amebainisha kuwa, mfumo wa eMrejesho toleo la pili (V2) ni toleo lililoboreshwa la jukwaa la kidigitali linalotumia akili mnemba (AI) kukusanya, kuchambua, na kutoa mrejesho wa haraka kwa wananchi kuhusu huduma wanazozipokea kutoka taasisi za Serikali na mashirika ya Umma.