MKURUGENZI Mtendaji wa Kiwanda cha kutengeneza vioo cha KEDA kilichopo Mbezi Msufini, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Tony Wu, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira mazuri yanayowavutia wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, Ismail Ally Ussi, Wu alisema ni heshima kubwa kwa kiwanda cha KEDA kutembelewa na Mwenge wa Uhuru.
“Ni heshima kubwa kwa kiwanda chetu cha KEDA kutembelewa na Mwenge wa Uhuru. Hii ni ishara ya kutambua mchango wetu katika maendeleo ya Taifa,” alisema Wu.
Alieleza kuwa uamuzi wa kuwekeza Tanzania ulitokana na sera nzuri za uwekezaji, mazingira rafiki ya kodi pamoja na soko kubwa kutokana na idadi ya watu waliopo nchini. Alisema kuwa hadi sasa, uwekezaji katika kiwanda hicho umegharimu takribani Shilingi bilioni 9 za Kitanzania.
Wu aliongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho umeleta fursa za ajira kwa wakazi wa Mkuranga, ambapo zaidi ya watu 500 wameajiriwa moja kwa moja. Vioo vinavyozalishwa huuzwa ndani ya Tanzania na nje ya nchi, huku asilimia 20 ya bidhaa zikielekezwa kwenye soko la Afrika Mashariki na asilimia nyingine kusambazwa katika mataifa mbalimbali.
“Kiwanda hiki kimekuwa kikishiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kijamii, zikiwemo taasisi za Serikali,” alibainisha Wu.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ally Ussi, alisema Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa maeneo yenye viwanda vingi vinavyochangia ajira kwa vijana na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
“Kiwanda hiki kinazalisha vioo vyenye ubora wa hali ya juu na kusafirisha hadi nje ya nchi. Wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na wawekezaji kama hawa kwa ustawi wa Taifa,” alisema Ussi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED