PURA yashiriki ukaguzi, majaribio mtambo kuchimba visima vya gesi asilia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:32 PM Jul 21 2025
PURA yashiriki ukaguzi, majaribio mtambo kuchimba visima vya gesi asilia
Picha:Mpigapicha Wetu
PURA yashiriki ukaguzi, majaribio mtambo kuchimba visima vya gesi asilia

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeshiriki kazi ya ukaguzi na majaribio ya mtambo utakaotumika kuchimba visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara.

Ukaguzi huo ambao umefanyika katika Jimbo la Tianjin nchini China, umelenga kuhakiki uimara na ufanisi wa mtambo huo kabla ya kusafirishwa nchini Tanzania kwa kazi ya uchimbaji wa visima vya gesi asilia inayotarajiwa kuanza Novemba 2025.

Pamoja na ukaguzi wa mtambo huo wenye uwezo wa kuchimba hadi urefu wa mita 8000, PURA pia ilishiriki kama muangalizi katika ukaguzi na majaribio ya mifumo mbalimbali iliyopo katika mtambo huo na mabomba yatakayotumika wakati wa uchimbaji.

Kwa mujibu wa PURA, hatua hiyo ya ukaguzi ni muhimu kwa kuwa inatoa hakikisho la ufanisi wa mtambo kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi.

PURA, kama mdhibiti wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli nchini inashiriki na kusimamia hatua zote za mradi kuhakikisha mradi unatekelezwa kama ulivyopangwa.

Inatarajiwa kuwa, visima vitakavyochimbwa vitaongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku.