RC Mtanda: W'biashara tumieni Dawati Maalumu la Biashara

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:55 PM Sep 03 2025

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wafanyabiashara kutumia kikamilifu Dawati Maalumu la Uwezeshaji Biashara kwa Maendeleo ya Taifa, lililozinduliwa rasmi leo jijini Mwanza, kwa lengo la kusaidia kutatua changamoto zao na kuongeza ufanisi wa biashara.

Mtanda amesisitiza umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kuchangia kulingana na uwezo wake. Pia aliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha dawati hilo linafika hadi ngazi ya wilaya ili kuwafikia wafanyabiashara wote.

“Suala la kodi ni suala la kitaifa, hatutaweza kuiendesha Serikali bila kulipa kodi. Maendeleo tunayoyaona sasa, kwa mfano daraja la Kigongo–Busisi lililozinduliwa hivi karibuni, yote ni matokeo ya kodi tunazolipa sisi wenyewe,” amesema Mtanda.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Faustine Mdesa, amesema dawati hilo si kwa ajili ya kutoza kodi bali kutoa msaada, kusikiliza changamoto na kuboresha ushirikiano kati ya TRA na walipa kodi.

“Kuanzishwa kwa dawati hili ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kuboresha mahusiano ya kikazi kati ya TRA na walipa kodi ili kuongeza ulipaji wa hiari. Dawati hili ni maalumu kwa ajili ya kuwatambua, kuwasikiliza na kuwawezesha walipa kodi. Halihusiani na utozaji kodi bali ni sehemu ya msaada na suluhisho kwa walipa kodi wadogo na wakubwa,” amefafanua Mdesa.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Mwanza, Jacob Paul, alisema dawati hilo limewapa matumaini mapya na ni fursa ya kutatua kero walizokuwa wakikabiliana nazo kwa muda mrefu.

“Tumekuwa na kero nyingi bila sehemu rasmi ya kuziwasilisha. Sasa tumepata sehemu sahihi ya kusaidiwa na tumeahidi kulitumia kikamilifu kupata suluhisho la changamoto zetu,” amesema Paul.