Serikali yataka wafanyabiashara kushiriki EXPO 2025

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:23 PM Apr 24 2025
Serikali yataka wafanyabiashara kushiriki EXPO 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Serikali yataka wafanyabiashara kushiriki EXPO 2025

Serikali imelipongeza Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kuandaa vyema uratibu wa Maonesho ya Kimataifa ya Wazalishaji yajulikanayo kama TIMEXPO 2025.

Maonyesho hayo yatafanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Novemba mwaka huu  katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam na yanatarajiwa kuhudhuriwa na waonyeshaji 400 na watembeleaji zaidi ya 35,000.

Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Suleiman Serera, wakati wa hafla ya uzinduzi wa maonyesho hayo ya kimataifa. 

Dk Serera amesema amefurahishwa na namna CTI na TANTRADE walivyojipanga kuhakikisha maonyesho hayo yanafana na kuwasaidia wazalishaji wa ndani kuonyesha bidhaa zao kimataifa.

Aidha, amesema Tanzania inazidi kupanda chini ya  uongozi shupavu na wenye maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa  Serikali kuendelea kutekeleza mageuzi ya kina ili kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani, shirikishi na unaoendeshwa na teknolojia.

 “Tunawekeza kwenye miundombinu. Tunafanya nishati ya kisasa, kuwezesha biashara, na kuweka dijitali. Tunapunguza gharama za kufanya biashara na kufanya kazi bila kuchoka ili kuiweka Tanzania kama kitovu cha viwanda kwa Afrika Mashariki na Kusini,” alisema. 

Amesema marekebisho yaliyofanyika siyo ya mapambo kwani yanalenga kufungua fursa, kuvutia uwekezaji, na kutoa kazi zenye staha kwa watanzania. 

Amesema sekta ya viwanda nchini Tanzania inakua na uwekezaji mkubwa umeendelea katika usindikaji wa mazao ya kilimo, vifungashio, dawa, nguo, vifaa vya ujenzi, na hata vifaa vya elektroniki. 

“Kupitia Mkakati Jumuishi wa Maendeleo ya Viwanda (IIDS), FYDP III, na marekebisho ya udhibiti, tunaendelea kuweka kipaumbele katika ukuaji wa viwanda kama njia ya ukuaji jumuishi na ushindani wa kimataifa,” alisema.

 Amesema Afrika sio tena bara la malighafi bali ni bara la masoko na watengenezaji wa bidhaa na kwamba kwa kuwa soko huru la Afrika AfCFTA linatumika sasa, watengenezaji wa bidhaa Tanzania  wanaweza kufikia watumiaji bilioni 1.4 katika bara zima.

3

 “Lakini ufikiaji pekee hautoshi lazima tuzalishe kwa kiwango kikubwa, chapa iliyo bor na kuuza nje kwa mkakati ndiyo maana  TIMEXPO ni muhimu kwaajili ya kuuambia ulimwengu kwamba kuna bidhaa zinatengenezwa Tanzania. Kama Mwalimu Julius Nyerere alivyowahi kusema: “Tanzania si maskini namimi leo nasema sisi ni matajiri,” amesema

 Naye Mkurugenzi Mtendaji wa (CTI) Leodegar Tenga amesema malengo ya maonyesho hayo ni kuonyesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.

 Amesema EXPO 2025 itasaidia kuonyesha fursa za maendeleo ya viwanda yaliyopo ili kuendelea kuvutiwa uwekezaji wa nje na kukuza viwanda vya ndani ikiwemo kupata wabia wa nje ya nchi.

“Rais amefanyakazi kubwa sana kwenye miaka yake minne amevutia uwekezajiwa pande zote duniani, tumeona mitaji inakuja kutoka nje, teknolojia mpya kwa hiyo nawahamasisha wenye viwanda waje kwenye maonyesho waonyeshe bidhaa zao,” amesema Tenga
4