Wastaafu, warithi kupewa mkono wa pole, mkupuo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:15 PM Apr 04 2025
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Yesaya Mwakifulefule.
Picha:Nipashe Digital
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Yesaya Mwakifulefule.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Yesaya Mwakifulefule amesema kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umeanzisha utaratibu wa kuwalipa mkono wa pole wa kiasi cha Sh. 500,000 tategemezi wa mstaafu aliyefariki ambazo hutolewa ndani ya siku 30.

Aidha, warithi wa mstaafu wanalipwa fedha za mkupuo wa miezi 36, jambo ambalo awali halikuwa linafanyika na kwamba bidhaa zote mbili zitazinduliwa hivi karibuni lengo likiwa ni kuwajali wanachama kwa nyakati zote.

Akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya PSSSF kwenye kuhudumia wanachama wakati wa Mkutano Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema kuna wanachama 15 hadi 20 waliopata mkono wa pole kutoka kwenye mfuko.

“Wastaafu wetu wanaishi muda mrefu na mfuko umeendelea kuhimili uwepo wao, tangu 2018 wakati mifuko inaunganishwa 124,000 leo tuna 176,000 hili ni ongezeko, na najua tukija mwakani wataongezeka, wote hawa wamestaafu na lazima waendelee kulipwa pensheni yao,”amefafanua.

Mwakifulefule amesema mwaka huu kuna bidhaa  kwa wastaafu wa serikali kuu walikuwa walikuwa wanapokea Sh. 20,000 au 25,000 lakini kwa maboresho ya sasa tangu Januari mosi wanapata wastani wa 150,000 kwa mwezi.

“Unaweza kuiona 150,000 kwa mwezi ni ndogo ila kukiangalia kinachotoka na kuingia kwa mwezi na kwa mwaka utaona ni fedha nyingi.Tangu unaajiriwa, unastaafu, unafariki PSSSF haikuachi hadi siku unapumzishwa kwenye nyumba ya milele,”amesema.