Katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, wadau mbalimbali wamejitokeza kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida ya kutumia nishati hiyo na madhara ya matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni.
Akizungumza na Nipashe Digital leo, Agosti 5, 2025, Mwenyekiti wa kikundi cha kumsemea Rais Samia katika Jimbo la Mbagala, Mwanaisha Katumbi, amesema wameamua kutoa elimu hiyo kwa wananchi ili kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya kulinda mazingira na afya ya jamii kupitia matumizi ya nishati safi.
“Tumegawa mitungi ya gesi na kutoa elimu ya namna ya kuitumia. Tumehimiza waliopokea wakawe mabalozi wa kuhamasisha wenzao kuacha kutumia mkaa na kuni,” amesema Katumbi.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo haziwezi kufanikiwa kikamilifu bila ushirikiano wa wadau wengine, na kuwataka wajitokeze kusaidia elimu na vifaa ili kufikia watu wengi zaidi.
Baadhi ya wananchi waliopokea mitungi ya gesi walieleza furaha yao na dhamira ya kuwa sehemu ya mabadiliko ya tabia katika jamii kuhusu matumizi ya nishati.
Zacharia Zablon, mmoja wa wanufaika, alisema: “Sijaoa, lakini nimepata mtungi wa gesi ukiwa umejaa. Nimeupokea kwa furaha. Ile tabu ya moshi na majivu niliyokuwa nikipata kupitia matumizi ya mkaa sasa imekwisha.”
Naye Hadija Abdallah, mkazi wa Mbagala Zakhem, amesema amejipanga vyema kwenda kuhamasisha matumizi ya nishati safi miongoni mwa wanawake wenzake.
Juhudi hizi zinaendana na maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa taifa linalotumia nishati salama, rafiki kwa mazingira na afya ya jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED