SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo, imeimarisha juhudi za kuleta mageuzi katika zao la mpunga nchini, kwa kuongeza bajeti ya wizara hiyo kutoka Sh. bil 294 mwaka 2020/2021 hadi zaidi trilioni 1.2 kwa mwaka huu wa fedha.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao, Usalama wa Chakula na Ushirika, Dk. Stephen Nindi, amesmea hayo wakati wa kongamano la wadau wa mpunga lililofanyika mjini Morogoro, lililohusisha wadau kutoka wizara mbalimbali, wakulima, watafiti, wawekezaji na mashirika ya umma.
Nindi amesema Serikali imeendelea kusimamia uanzishwaji na uendelezaji wa zaidi ya miradi 700 ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuongeza tija, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuondoa utegemezi wa kilimo cha mvua.
Amesema kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wanaendelea na maboresho kwenye skimu za umwagiliaji wakilenga kuongeza uzalishai na uhakika wa upatikanai wa mbegu bora.
Aidha, amesisitiza kuwa huduma za ugani, tafiti za kisayansi na matumizi ya mbegu bora ni maeneo mengine yanayopewa kipaumbele ili kuhakikisha mpunga unalimwa kwa ufanisi na kwa viwango vya kimataifa.
Katika kongamano hilo lililoshirikisha wadau wa mbegu za mpunga, umwagiliaji na biashara, Dk. Nindi akawahimiza wakulima kuchangamkia fursa hiyo ili kuendana na mahitaji pia kumudu ushindani wa soko la ndani na nje.
Baraza la Mchele Tanzania, limekuwa likifanya tafiti kuendeleza sekta ya mchele hiyo habata hivyo kupitia viongozi wake wanasema bado vipo vikwazo ikiwamo baadhi ya sheria na upatikanaji wa takwimu halisi za uzalishaji
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mchele Tanzania (RCT), Geofrey Rwiza, amepongeza jitihada za serikali katika kuwezesha sekta ya mpunga, lakini akaeleza kuwa bado kuna hitaji la kuwekeza zaidi katika mifumo ya upatikanaji wa takwimu sahihi za uzalishaji na usimamizi wa masoko na mazingira yasiyo Rafiki ya biashara ya mchele, ili kuwawezesha wakulima kunufaika ipasavyo pamoja na ushuru mkubwa wa mazao kwa halmashauri.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, amesema baadhi ya changamoto katika sekta hiyo zinatokana na ukosefu wa uratibu wa kutosha miongoni mwa wadau wa mnyororo wa thamani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED