Mjue Boniface Mwangi, aliyefutiwa mashtaka ya ugaidi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:22 PM Jul 21 2025
Boniface Mwangi
Picha: BBC
Boniface Mwangi

IDARA ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kenya, imetupilia mbali mashtaka yanayohusiana na ugaidi yaliyofungiliwa dhidi ya mwanaharakati Boniface Mwangi.

Mwangi sasa anakabiliwa na mashtaka mawili, ikiwa ni pamoja na kumiliki silaha bila kibali na kupatikana na sumu pamoja na vitoa machozi.

Alikana shtaka hilo na kuachiliwa kwa bondi ya shilingi milioni moja za Kenya.

Kukamatwa kwake kumelaaniwa, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakikosoa kuwa ni kwa lengo la kukandamiza sauti za upinzani.

Mwanaharakati huyo amekanusha tuhuma hizo, akisema katika chapisho kwenye X: "Mimi sio gaidi."

Tuhuma zinazohusishwa na maandamano ya Juni 25, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) inayofadhiliwa na serikali.

Watu 19 walikufa wakati waandamanaji walipopambana na polisi. Mamia pia walijeruhiwa na mali na biashara kuharibiwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen ameeleza maandamano hayo kama "ugaidi uliojificha kama upinzani" na "jaribio lisilo la kikatiba" la kuiangusha serikali.

Watu 38 zaidi waliuawa katika maandamano yaliyofuata mapema mwezi huu, KNHCR imesema.

Tangu Juni mwaka jana, zaidi ya watu 100 wameuawa katika wimbi la maandamano ya kupinga serikali, huku polisi wakituhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano.

Mwanaharakati huyo, pia aliwahi kushikiliwa na jeshi la polisi Tanzania, na kuachiliwa huru, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Haki Afrika aliiambia BBC.

Hussein Khalid alithibitisha kuwa alikuwa pamoja na Mwangi wakiwa njiani kutoka Mombasa na sasa wanaelekea Nairobi.

Waziri Mkuu na Katibu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, awali alikuwa pia ametangaza kuachiliwa kwa mwanaharakati huyo karibu na eneo la mpaka kati ya nchi hizo mbili ambaye alikuwa amekamatwa nchini Tanzania kwa siku kadhaa.

Mudavadi, katika taarifa yake, alisema Mwangi aliachiliwa huru Alhamisi asubuhi na mamlaka ya Tanzania baada ya serikali kuingilia kati.

Hata hivyo, hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu hali yake ya afya hadi kufikia sasa.

Mwangi alikamatwa na polisi Mei 2019, kwa madai ya kuandaa mapinduzi nchini Kenya

Maofisa wa upelelezi walikuwa wamemkamata Mwangi nyumbani kwake na kumpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako alirekodi taarifa.

Aliachiliwa muda mfupi baada ya taarifa inayoelezea mashtaka ambayo huenda akakabiliwa nayo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwaka 2024 Kuzuiliwa kwake kulikuja baada ya kuitisha maandamano dhidi ya serikali katika mbio za marathon katika mji mkuu, Nairobi.

Polisi walikuwa wamethibitisha kuwa Mwangi alikuwa kizuizini lakini hawakutoa maelezo zaidi.

Kuzuiliwa kwake kulizua hasira miongoni mwa wafuasi wake, waliotaka aachiliwe.

Alikuwa akikusanya watu kwenye X (zamani Twitter) kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu, akitumia neno #RutoMustGo na #OccupyStanChart,

Aliwataka watu kuvalia rangi za bendera ya taifa, kuvaa kanga zenye ujumbe "RutoMustGo" na kushiriki maandamano mtandaoni.

Chanzo: BBC