RAIS wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, amesema anajivunia usajili wa aliyekuwa Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala, kuwa utaongeza mafanikio zaidi kutokana na ubora wake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, alisema Tshabalala ni miongoni mwa wachezaji wazuri hapa nchini na kuweka wazi alikuwa anampenda sana beki huyo wa kushoto.
"Najivunia sana uwapo wa Mohamed Hussein kwenye timu yetu kwa kuwa ni mchezaji ambaye hakuna asiyetamani kuwa naye kutokana na ubora wake," Hersi
Alisema mbali na nyota huyo wataendelea kutangaza wachezaji waliowasajili pamoja na wale watakaoachana nao.
Hersi alisema malengo yao ni kusajili wachezaji wenye viwango vya juu ili kuendeleza ushindani walioufanya msimu uliopita.
Aidha, aliwaomba mashabiki wao kuendelee kuwapa ushirikiano katika kipindi hiki ambacho wanafanya usajili kwa ajili ya kuboresha zaidi kikosi chao.
Alisema kutokana na malengo hayo, anaamini watafanya vizuri na kwamba wataingia kambini mapema ili kuanza maandalizi kuelekea msimu huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Kwa upande wa Msemaji wa timu hiyo, Ally Kamwe, alisema wiki hii wataanza kutangaza rasmi wale wanaoachana nao pamoja na wale waliowasajili.
Alisema msimu ujao utakuwa mgumu zaidi, hivyo watauanza wakihakikisha wanatetea makombe yao yote kwa kushinda michezo watakayoicheza.
"Tumejipanga vizuri kwenye suala la usajili huwa hatukurupuki, tunasajili vifaa ambavyo tunaamini vitaleta mapinduzi kwenye timu yetu na kuwapa burudani mashabiki wetu," alisema Kamwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED