ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi, amesema kushiriki Uchaguzi Mkuu ni haki ya kikatiba ambayo wananchi hutegemea waliowachagua wana dhamana ya kutawala na kuongoza nchi.
Amesisitiza dhamira hiyo ikiambatana na uamuzi sahihi na hofu ya Mungu, akisema itasaidia kila mwanadamu kupima uamuzi wake.
Askofu Ruwa'ichi alisema hayo jana, kwenye Misa Takatifu ya Umoja wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Kuwategemeza Masista wa Shirika la Dada Wadogo, Visiga, mkoani Pwani, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.
Alisema kuelekea Uchaguzi Mkuu, watu wote, wakiwamo wapigakura na wapigiwa kura, waongozwe na dhamira safi, hai yenye ukweli na kuzingatia hofu na utu wa mtu.
Aliomba serikali kuwasikiliza wananchi wenye malalamiko, kuhusu haki yao hususan ya kisiasa na kwamba unyenyekevu huanza kwa kujengwa kwenye ukweli na uwazi, unaobeba haki, kuwajibika mbele ya Mungu, akisisitiza kiongozi akiwa mnyenyekevu, mkweli, ataaminika na watu wote.
Kadhalika, alivitaka vyama vya siasa pamoja na serikali, vihakikishe kunakuwapo haki za wananchi kwa kuwa nguvu ya kundi hilo, imo hasa kwenye hoja, na si mabavu.
“Mpigakura na mpigiwa kura mnaalikwa kuheshimu dhamira juu ya suala hili la uchaguzi mkuu usirubuniwe kwa vitisho, wala kwa rushwa, kwa namna yoyote ile.
“Naiomba serikali na wenye mawazo tofauti ya masuala ya uchaguzi, muongozwe na utamaduni wa mazungumzo katika kutekeleza haki, kwa mujibu wa Ibara ya 21 (Katiba).
“Kwenye uchaguzi mkuu, nawaomba raia wote kuongozwa na dhamiri iliyo safi, iliyo hai na kuongozwa na ukweli halisi, wenye kuzingatia hofu ya Mungu na historia ya nchi yetu.”
Pia, alieleza ulivyo uzoefu wa uchaguzi nchini, hasa zilizopita baada ya uhuru, tangu mwaka 1962 hadi mwaka 2015, akizitaja kwamba zilithibitika, ziliaminika na viongozi wakapatikana, hata kama zilikuwako changamoto kadhaa.
“Serikali kupuuza wanaolalamika, si afya wala tija kwa taifa letu. Wakati uliokubalika kuzungumza ni sasa, na wala hamjachelewa, hatuchelewi kujisahihisha, wala kutenda mema.”
“Siku ya Mwalimu, Nyerere, tunapomkumbuka Baba wa Taifa, tuyatafakari juu ya watanzania na ustawi wake. Kiongozi wa watu akiwa mnyenyekevu, mkweli na kuaminika na watu wote…Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaweka wazi kuwa mamlaka ya nchi yamo chini ya wananchi na serikali kuwajibika kwa wananchi, serikali ikiwa na wajibu kulea na kuleta ustawi wa watu wote, bila ubaguzi,” alisema.
Akizungumzia suala la watu kutekwa na kupotea, alisema kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, linasikitisha.
“Utekaji huu umesababisha haki ya msingi ya uhai kupotea, hakuna kulaani utekaji, kwa miaka kadhaa matukio haya yamekithiri, ikumbukwe uhai wa kila mwanadamu unadhihirisha utukufu wa Mungu, mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu, hakuna mwenye haki ya kumwondolea uhai wake, kazi ya serikali ni kulinda uhai wa kila mwanadamu.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzaniza, kila mtu ana haki ya msingi na inalindwa kwa gharama zozote, tunataka serikali kuhakikishaia raia usalama wa uhai, bila ubaguzi wowote,” alisema Askofu Ruwa'ichi.
Alisema wagombea na vyama vyao wanapaswa kuonesha uwezo wa kuwashinda wanaoitwa watekaji na kushughulikia uhalifu, kwa kuzingatiwa utawala wa kisheria.
“Ninawatakieni Uchaguzi Mkuu wa haki, ukweli, uhuru na wa kuaminika mwaka huu 2025,” alisema Askofu Ruwa'ichi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED