Askofu Shoo: Mamlaka, wanaosimamia uchaguzi mkuu sikilizeni sauti za wananchi

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 10:10 AM Apr 20 2025
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo
Picha: Mtandao
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo

ASKOFU wa Dayosisi ya Kaskazini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo, amewataka wenye mamlaka na wahusika wote wanaosimamia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kusikiliza sauti za wananchi na viongozi juu na wadau wengine wanaoitakia mema Tanzania.

Akitoa salamu za ujumbe wa Pasaka jana katika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi Mjini, Askofu Shoo, amesema viongozi wa dini wameshatoa wito kwamba, ni haki na wajibu wa raia kuchagua viongozi wanaowataka, huku akihimiza uchaguzi huo  usiingiliwe na mamlaka iwayo yote.

"Waacheni watu wachague kwa uhuru viongozi wanaowataka. Tunaomba sana uchaguzi huu usifanane na chaguzi nyingine zilizopita. Ule wa 2019, 2020 na huu uliofanyika mwaka jana (2024), Hatutaki kuona yale yaliyotokea katika chaguzi nilizozitaja.

"Hatutaki kuona yanajirudia ndugu zangu. Tunaomba wananchi wote msikilize sauti hii. Wenye mamlaka  na wahusika wote katika zoezi zima hili la uchaguzi mkuu wazingatie hayo.

...niwaombe wenye mamlaka na wanaosimamia uchaguzi huu, kusikiliza sauti za wananchi. Sikilizeni sauti za viongozi wa juu na wadau wengine wanaoitakia nchi hii mema. 

Msizibe masikio, mlitutaka tutoe ushauri, tutoe maoni, tumetoa maoni, heshimuni maoni ya Watanzania. Tutaendelea kusema na mwenye kusikia asikie."