MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini fedha za miradi Sh. milioni 635.44 zilikopwa na kutorejeshwa.
Aidha, amependekeza menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia irejeshe haraka kwenye miradi husika fedha zilizokopwa ili kuepuka usumbufu katika utekelezaji wa shughuli zilizopangwa za miradi.
Katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24 kipengele cha usimamizi wa fedha, matumizi na bajeti, amesema kushindwa kurejesha fedha kwenye miradi husika kunakwamisha ufikiaji wa malengo ya miradi hiyo.
Hatua hiyo inaweza kusababisha ucheleweshaji katika utekelezaji wa shughuli zilizokusudiwa za miradi.
Miradi ambayo fedha zilikopwa ni Mkataba wa Ufadhili wa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) wa tarehe 21 Mei mwaka 2020.
Aidha, anasema sehemu ndogo ya nne ya sehemu ya pili ya Mkataba wa Ufadhili wa Mradi wa Ujenzi wa Ujuzi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EASTRIP) inataka fedha za miradi zitumike kufanikisha malengo ya miradi hiyo na kwamba watekelezaji wanapaswa kuzingatia mikataba ya ufadhili ili kuhakikisha kuwa fedha zinatumiwa tu kwa shughuli zilizokusudiwa za mradi.
“Hata hivyo, wakati wa ukaguzi nilibaini kuwa katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia ilikopa Sh. 635,447,342 kutoka katika miradi ya EASTRIP wa kutekeleza shughuli za Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia Sh. 135,447,580 na SEQUIP kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia 499,999,762.
“Hatua hii ilikiuka sheria na masharti yaliyobainishwa katika mikataba ya fedha za miradi na miongozo ya utekelezaji wa miradi inayosimamia uendeshaji wa miradi hii.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED