Blisspals Tanzania yatoa wito kupambana na upweke kwa wazee

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 10:39 AM Sep 01 2025
Blisspals Tanzania yatoa wito kupambana na upweke kwa wazee
Picha: Imani Nathaniel
Blisspals Tanzania yatoa wito kupambana na upweke kwa wazee

Chama cha Wazee Wastaafu cha Blisspals Tanzania Limited, kinachojihusisha na masuala ya afya za wazee, kimeitaka jamii kuhakikisha inawalinda wazee dhidi ya changamoto ya upweke, hali ambayo mara nyingi husababisha maradhi mbalimbali yakiwemo ya moyo.

Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam katika mkutano wa pamoja wa wahudumu wa afya waliotumikia muda mrefu na wastaafu. Katika kikao hicho ilibainika kuwa tatizo la upweke ni miongoni mwa vyanzo vya kuongezeka kwa magonjwa kwa wazee.

Aidha, chama hicho hutoa huduma mbalimbali za kiafya kwa kuwafuata wazee majumbani, bila kuwatenganisha na familia zao.

Akizungumza katika mkutano huo, Florence Temu, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Blisspals Tanzania, alisema mikusanyiko ya wastaafu inalenga kukumbushana umuhimu wa kuishi maisha bora ya uzee.

“Unapostaafu katika sekta ya afya wewe ni hazina kwa Taifa. Bado unafaa kulitumikia kwa hekima na uzoefu wako,” alisema Temu.

Kwa upande wake, Dkt. Ali Nzige, daktari mstaafu, aliitaka Serikali kuandaa sera maalum ya kuwatambua na kuwathamini wazee kutokana na mchango wao mkubwa katika jamii.

“Ni vyema wazee wakapewa huduma stahiki na kuwekewa mazingira rafiki kwa ajili ya afya zao,” alisisitiza Nzige.

Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili, Delila Kimambo, alisema kuna maisha mapya baada ya kustaafu, hivyo ni muhimu kwa wazee kuzingatia ulaji bora, kufanya mazoezi na kushirikiana na wenzao ili kuondoa upweke.

“Kukusanyika pamoja husaidia kuongeza furaha na kuimarisha afya ya mstaafu. Kushauriana na kushirikiana ni busara inayoweza kuongeza muda wa kuishi,” alisema Kimambo.