Mgombea urais CCM kufanya mikutano minne Mbeya

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 05:58 PM Sep 01 2025
Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Langael Akyoo
Picha: Nebart Msokwa
Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Langael Akyoo

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili mkoani Mbeya, yenye lengo la kunadi sera za chama hicho.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Langael Akyoo, ameyasema hayo alipozungumza na wandishi wa habari kuhusu maandalizi ya ziara hiyo, amewataka wananchi kujitokeza kwenda kusikiliza sera za chma hicho.

Amesema Dk. Samia atafanya mikutano minne ya kampeni kwenye wilaya nne za mkoa huo ambazo ni Mbeya Vijijini, Mbeya Mjini, Rungwe na Mbarali kabla ya kuelekea mkoani Njombe.

“Sisi mtaji wetu ni wanachama, tuna makundi mbalimbali ya wanachama kuanzia ngazi ya mabalozi, lakini kwenye mikutano yetu hii tunawaomba wananchi wote wa mkoa huu hata ambao sio wanachama wajitokeze kuja kusikiliza sera zetu,” amesema Akyoo.

Amesema serikali ya chama hicho imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo na kwamba Ilani ya Uchaguzi ya mwaka huu, imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.