MWANAUME mmoja ambaye hajafahamika jina wala makazi yake amekutwa amefariki dunia katika Bwawa la mji linalomilikiwa na Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) lililopo kata ya Nyihogo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilayani Kahama, Mrakibu Msaidizi Stanley Luhwago amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea August 30 majira ya saa tatu asubuhi mwaka huu na alipokea taarifa kutoka kwa mmoja wa mashuhuda aliyeona mwili ukiwa unaelea.
Amesema, walifika eneo la tukio na kukuta watu wengi ambao walishirikiana nao pamoja katika zoezi la kuutafuta mwili huo na bwawa lilikuwa na magugu maji mengi lakini walifanikiwa kuopoa mwili huo majira ya mchana.
Aidha, amesema, mwili wameukabidhi Jeshi la Polisi na kuupeleka katika hospitali ya manispa ya kahama kwa ajili ya kuuhifadhi na mpaka sasa marehemu hajafahamika jina, umri wala makazi yake na ndugu watakapopatikana watakabidhiwa kwa hatua za mazishi.
Luhwago amewataka wananchi kufukia madibwi au mashimo ya vyoo wanayochimba na ujenzi wake haujakamilika ili kuzuia watu kutumbukia nyakati za usiku na wale wenye visima waweke mfuniko ili kuzuia watoto wadogo hasa wanaotambaa kuingia na kusababisha maafa.
Mkazi wa Nyihogo Edward James ameomba serikali kulizungushia eneo hilo uzio ili kuzuia watoto kuingia na kuogelea hovyo na awali kulikuwa wazi na kila mmoja aliyekuwa akisogea alikuwa akionekana na kuondolewa lakini kwa sasa limezunguka na miti ya kupandwa hivyo ni ngumu kuwaona watu.
Nae Braiton Polengile amesema,kwakuwa hakuna mradi unaotekelezwa kupitia bwawa hilo wala usimamizi, lingefungwa ili kuzuia watu kuendelea kuingia kwani tukio hili sio la kwanza kutokea na hata mwaka uliopita uliokotwa mwili wa marehemu ukiwa unaelea bwawani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED