Mwenge wa Uhuru kukagua miradi ya Sh bilioni 164 Geita

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:02 PM Aug 30 2025
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela

Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 61 ya maendeleo mkoani Geita yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 164.

Mwenge huo utaingia mkoani humo Septemba 1, 2025, ukitokea Mwanza na utakimbizwa katika wilaya tano na halmashauri sita za mkoa huo. Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, amesema thamani ya miradi itakayokaguliwa mwaka huu imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 500 ikilinganishwa na mwaka 2024, ambapo miradi 65 yenye thamani ya Sh bilioni 32 ilitembelewa.

“Ongezeko hili linaashiria kasi ya uwekezaji na maendeleo katika mkoa wetu. Mwenge wa mwaka huu utachochea zaidi maendeleo kutokana na thamani kubwa ya miradi itakayokaguliwa,” amesema Shigela.

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea mwenge na kushiriki shughuli mbalimbali zitakazofanyika sambamba na mbio hizo.

Aidha, Shigela amesema mbio za mwaka huu zinabeba ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura na kushiriki kampeni kwa amani ili kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo.

“Kila mgombea atapewa nafasi ya kufanya kampeni bila usumbufu. Ni wajibu wetu kushiriki kwa wingi tusikilize sera za wagombea na kufanya maamuzi kwa atakaetuletea maendeleo,” ameongeza.

Mbio za Mwenge wa Uhuru zitapita mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na kuhitimishwa Oktoba 14, siku ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.