Liverpool imefikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji wa Sweden, Alexander Isak kutoka Newcastle United kwa ada ya pauni milioni 125, ambayo ni rekodi mpya ya usajili nchini Uingereza. Newcastle wamedokeza kuwa thamani ya mkataba huo inaweza kufikia pauni milioni 130 endapo masharti ya nyongeza yatakamilika.
Leo Jumatatu Septemba 01,2025 dirisha kuu la usajili majira ya joto litafungwa usiku. Isak (25) ameonekana katika viunga vya klabu ya Liverpool ambapo inaelezwa anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba wa miaka sita na Liverpool. Awali, Liverpool walikataa kwa ofa ya pauni milioni 110 mwezi Agosti, lakini hatimaye wamefanikiwa kumpata mshambuliaji waliomlenga kama chaguo lao kuu majira haya ya kiangazi.
Liverpool tayari wameshavunja rekodi ya usajili wao kwa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Ujerumani, Florian Wirtz kwa pauni milioni 100 (na nyongeza ya milioni 16). Kupatikana kwa Isak kutafanya gharama za klabu kufikia zaidi ya pauni milioni 416 msimu huu wa usajili, kiwango cha juu zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England.
Wakati huo huo, klabu hiyo pia imepata mapato ya takribani pauni milioni 190 kupitia mauzo ya wachezaji akiwemo Luis Diaz, Darwin Nunez, Trent Alexander-Arnold na wengineo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED