Marufuku kumbi za starehe, nyumba za ibada kupiga muziki

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 06:10 PM Sep 01 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Frank Nkinda
Picha: Shaban Njia
Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Frank Nkinda

MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Frank Nkinda amewatangazia wamiliki wa kumbi za starehe yakiwamo madhehebu ya kidini, yanayopiga kelele za muziki mpaka saa tisa usiku, ni marufuku, kwa kuwa wanasababisha wananchi kushindwa kupumzika kutokana na kelele hizo.

Nkinda ameyabainisha haya leo, wakati mkutano wake wa hadhara wa kurejesha majibu ya maswali aliyokuwa ameulizwa na wananchi katika mkutano kwenye viwanja vya maegesho ya magari ya mizigo kata ya Majengo manispaa ya kahama.

Amesema si sawa biashara kuwa kikwazo kwa watu wengine hivyo mwisho wa kupiga muziki sauti ya juu, iwe saa sita usiku na sio kukesha nao na kuwasumbua wananchi na kuyataka madhebu ya kilokole pia kupunguza sauti za vyombo vyao kwa wakati huo.

Wananchi
“Ninakuagiza Ofisa Utamaduni kulisimamia suala hili lisiendelee kuwa kero kwa wananachi na wale watakaobainika kwenda kinyume na hili wachukuliwe hatua za kisheria, wananchi wanashindwa kupumzika usiku kwasababu ya kelele za mziki usiokuwa tija,” ameongeza Nkinda.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Majengo, Mustapha Mayala amesema, kelele hizo zinasababisha hata wanafunzi kushindwa kujisomea nyakati za usiku pamoja na wenye presha, kuanguka hovyo na kuhatarisha maisha yao huku nyingi zikitoka kwenye kumbi za starehe na nyumba za ibada.