Watu wawili wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa huku nyumba kadhaa zikiharibiwa kufuatia mlipuko uliotokea katika banda la kuchomelea vyuma lililopo Kichemuchemu, Kata ya Magomeni, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Imeelezwa kuwa kibanda hicho, kilichokuwa kikitumika kwa shughuli za kuchomelea vyuma na kujengwa kwa tofali, nacho kilibomoka kutokana na nguvu ya mlipuko huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, akizungumza Agosti 31 ofisini kwake Kibaha, alisema mlipuko huo ulitokea majira ya saa moja asubuhi.
Morcase aliwataja waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Dotto Mrisho (24), fundi wa kuchomelea mkazi wa Kichemuchemu, na Said Ramadhani (53) mkazi wa Sanzale, huku Hassan Omari akijeruhiwa.
Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mlipuko huo kilihusiana na chuma alichokuwa anakata Dotto Mrisho wakati akifanya kazi yake.
Amesema kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kubaini kwa undani chanzo cha mlipuko huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED