Dk. Samia ataja mkakati kumaliza foleni malori Tunduma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:12 PM Sep 03 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake inapanga kuendeleza ukarabati na upanuzi wa barabara kuu inayounganisha Tanzania na Zambia yenye urefu wa kilomita 75, ili kupunguza msongamano wa malori Tunduma mkoani Songwe.

Dk Samia ameyasema hayo leo, Jumatano Septemba 3, 2025 alipozungumza na wananchi wa Tunduma mkoani Songwe, wakati wa mkutano wake wa kampeni za kugombea urais.

Amesema upanuzi wa barabara hiyo, unalenga kuifanya iwe ya njia nne, ili kurahisisha usafiri na usafirishaji na hatimaye kumaliza changamoto ya msongamano wa malori katika eneo hilo.

Jambo lingine aliloahidi kulifanya ili kumaliza msongamano huo, amesema ni kukarabati Reli ya Tazara na tayari mkataba umeshasainiwa na China kufanikisha kazi hiyo na hivyo, kufanikisha usafirishaji haraka wa mizigo.

Utekelezwaji wa hayo, kwa mujibu wa Dk. Samia, utaambatana na ujenzi wa Bandari Kavu yeye ukubwa wa ekari 1,800 katika eneo la Katenjele, Kata ya Mpemba ili malori yasiegeshwe barabarani.

Barabara mbadala, amesema itaongezwa kuanzia eneo la Mwakabanga nae neo la maegesho na mizani ili malori yapime haraka na kuondoka badala ya kusimama kwenye foleni.

“Tutahakikisha nyaraka zinachakatwa kabla ya magari kufika mpakani ili kupunguza muda ambao malori yanautumia kusubiria hapa,” amesema.


Sambamba na hayo, amesema Serikali ya Tanzania na Zambia zimeshaanza mazungumzo kuhakikisha mamlaka inayokusanya mapato nchini humo ifanye kazi kwa saa 24, ili kurahisisha uvukaji.