MAHAKAMA Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imempa ahueni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, baada ya kuruhusu maelezo ya maandishi ya shahidi wa upande wa Jamhuri kutumika kama kielelezo cha utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, baada ya mahakama kutupilia mbali pingamizi la upande wa Jamhuri lililodai kuwa Lissu hakufuata utaratibu unaotakiwa kisheria.
Mahakama ilieleza kuwa Lissu alifuata taratibu zote za kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 163 cha Sheria ya Ushahidi (TEA) na uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi kadhaa zilizotolewa kama rejea.
“Mahakama imejiridhisha kuwa mshtakiwa alifuata taratibu zinazotakiwa kisheria katika kuomba maelezo hayo yakubaliwe kama kielelezo cha upande wa utetezi. Kwa hiyo, pingamizi la Jamhuri linatupiliwa mbali,” alisema Jaji Ndunguru akisoma uamuzi wa jopo hilo.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, maelezo ya shahidi wa Jamhuri, Mkaguzi wa Polisi John Kaaya, sasa yamesajiliwa rasmi kama kielelezo cha kwanza cha upande wa utetezi (DE1).
Awali, mahakama hiyo ilikuwa imekataa ombi kama hilo la Lissu kuhusu maelezo ya ACP George Bagyemu, Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum Dar es Salaam, lakini safari hii Lissu alirekebisha hoja zake na kufuata maelekezo ya Mahakama ya Rufani, jambo lililompa ushindi huo mdogo lakini wenye uzito mkubwa katika kesi hiyo.
“Mahakama imeangalia na kuzingatia utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa kifungu cha 163 cha Sheria ya Ushahidi (TEA) na uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Lilian Jesus Fortes, Shadrack Sospeter dhidi ya Jamhuri,” alisema Jaji Ndunguru.
KIINI CHA MVUTANO
Katika hoja zake, Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Zegeli alidai kuwa Lissu alishindwa kufuata taratibu za kuomba maelezo hayo yakubaliwe kama kielelezo, akidai alipaswa kuonesha maeneo maalum ya mkinzano kati ya aliyosema shahidi na aliyoyaandika.
Hata hivyo, mahakama haikuridhishwa na hoja hiyo, ikibainisha kuwa Lissu aliainisha maeneo 43 aliyokusudia kumhoj hahidi na kuyawasilisha kwa mujibu wa sheria.
Baada ya uamuzi huo, Lissu aliendelea kumhoji shahidi huyo, akitumia maelezo yake ya awali kama rejea, hatua iliyozua mvuto mkubwa katika ukumbi wa mahakama. Katika maswali yake, Lissu alitaka kujua kama video iliyosababisha mashtaka hayo ilirekodiwa katika mkutano wa CHADEMA uliofanyika Mikocheni, ambao ulirushwa mbashara kupitia televisheni na mitandao ya kijamii kama Jambo TV, Mwanzo TV, Clouds Media na The Chanzo TV.
Shahidi alikiri kuwa hakufanya upelelezi wa kina kuhusu mitandao hiyo na kwamba hakufahamu kama Lissu ndiye aliyeandaa, kurekodi au kusambaza video hiyo. “Sikufanya upelelezi wa mitandao mingine. Hivyo, siwezi kusema ni nani hasa aliyerusha matangazo hayo,” alijibu shahidi kwa tahadhari.
Katika kipindi cha maswali na majibu, Lissu alihoji sababu za watu wengine waliokuwa kwenye mkutano huo kutoshtakiwa, vikiwamo vyombo vya habari vilivyorusha matangazo mbashara, jambo lililomfanya shahidi akiri kutokujua hatua za upelelezi dhidi yao. Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano, Lissu alipoendelea kumwuliza shahidi maswali ya dodoso kutokana na ushahidi wake aliotoa mahakamani Oktoba 9, 2025 huku akitumia maelezo halisi ya polisi ya shahidi huyo:
Lissu: Hii video ambayo ndiyo ilisababisha yote haya, ilirekodiwa kwenye mkutano wa tarehe 3 Aprili Mikocheni, Dar es Salaam? Kweli au si kweli?
Shahidi: Waheshimiwa majaji, sehemu iliporekodiwa sina ushahidi nayo.
Lissu: Ni kweli au si kweli mkutano huo uliofanyika Makao Mkauu ya CHADEMA, ulikuwa unarushwa mbashara Jambo TV YouTube, Mwanzo Tv, The Chanzo TV, Clouds n.k?
Shahidi: Sikupeleleza mitandao mingine.
Lissu: Katika ushahidi wako ulieleza kuwa huwa mnafanya doria mtandaoni saa 24 na kwamba huwa mnaachiana zamu. Ukasema ni kweli, kama hukuona huu mkutano uliorushwa mbashara. Nani alikuwapo zamu siku hiyo?
Shahidi: Kuwa zamu unaweza kuwa lakini kama anafuatulia kitu kingine, aliyekuwapo hakutoa taarifa ndiyo maana mimi nilivyobaini ndiyo nilikuwa mtu wa kwanza kuona na nikatoa taarifa.
Lissu: Nani aliyekuwa zamu siku hiyo?
Shahidi: Waheshimiwa majaji hili suala lazima nipitie kwenye kumbukumbu zangu niangalie ni nani aliyeingia siku hiyo, nisije nikatamka mtu kumbe siye, lakini ninawajua wote.
Lissu: Ahsante.
Lissu: Ni kweli au si kweli, hiyo picha ya mkutano wangu ilichapishwa na Arusha One Digital YouTube? Unasemaje hapo?
Shahidi: Sikumbuki.
Lissu: Kutokana na hayo unayoyakumbuka, hao watu walishiriki kusambaza hayo maneno, Clouds Instagram, Jambo Tv YouTube, ni sahihi au si sahihi kwamba kwa mujibu wa sheria yetu ya uhaini na wao wafanya kosa la uhaini?
Shahidi: Inategemea na upelelezi ulivyofanyika na ulivyobaini.
Lissu: Watu wanaosambaza maneno ya ugaidi, wakaanza kuyasamba lezi, kwa hiyo ya ugaidi siyafahamu.
Lissu: Unafahamu kama kuna kosa la kula njama kwemye ugaidi waliloshtakiwa nalo kina Bibi Titi Mohamed na wenzake? Shahidi: La kula njama lipo.
Lissu: Ni ushahidi sako kwamba mimi ndimi niliwaalika waandishi wa habari kuja kwenye mkutano wangu wa tarehe 3?
Shahidi: Hayo sikuyapeleleza.
Lissu: Unamfahamu ACP Bagyemu? Shahidi: Ndiyo, ninawafahamu.
Lissu: Kwenye ushahidi wake alieleza kwamba mimi ndimi niliita waandishi wa habari kwenye mkutano wangu.
Shahidi: Sikumsikia akitoa hayo maneno, sijui. Lissu: Wala hukupepeleza? Shahidi: Hayo unayoyatamka sikushirikishwa kupeleleza.
Lissu: Je, tuhuma dhidi yangu inasema nilizungumza na kuchapisha na kufanya tendo la hilo video ya kwenye Jambo TV. Wewe unasemaje?
Shahidi: Pale unapowaalika waandishi wa habari na kutoa taarifa mbele yao, unakuwa umeridhia taarifa hiyo kuchapishwa.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama mimi ni mmiliki wa Jambo TV.
Shahidi: Mmiliki simfahamu.
Lissu: Mimi ni Mkurugenzi wa Jambo TV?
Shahidi: Mkurugenzi simfahamu.
Lissu: Unafahamu kama mimi ni mwandishi wa habari wa Jambo TV?
Shahidi: Sifahamu kama wewe ni mwandishi wa habari za kwa watu wengine na wao wanakuwa wametenda kosa la ugaidi?
Shahidi: Sikufanya huo upele wa Jambo TV.
Lissu: Unafahamu kama mimi ni mfanyakazi wa aina yoyote wa Jambo TV?
Shahidi: Hilo sifahamu.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama mimi nilikuwa nimewaalika Jambo TV kuja kwenye mkutano wangu.
Shahidi: Hilo sifahamu.
Lissu: Waeleze kama mimi ndimi niliyeshikilia kamera.
Shahidi: Aliyekuwa anachukua hakuonekana.
Lissu: Mtu anayeita waandishi wa habari anakuwa ana mamlaka ya kuwaelekeza kwamba wanatakiwa kuandika hivi?
Shahidi: Hilo linategemea makubaliano yao ya ndani.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, hao waliorusha mbashara kama kuna hata mmoja ameshtakiwa na mimi kutenda kosa la uhaini.
Shahidi: Sifahamu Jambo TV au Clouds wapo upande gani katika hii kesi.
Lissu: Kwa nini waliosambaza hawajashtakiwa na mimi?
Shahidi: Katika uchunguzi wa kesi hii, Clouds na wengine sijui upelelezi ulifikia wapi na ulifanyikaje? Kwa sababu mpelelezi wa kesi yupo.
Lissu: Kweli au si kweli ule mkutano ulikuwa kati ya Mwenyekiti na watiania wa ubunge? Shahidi: Kutokana na kichwa cha habari cha maadhui yale, ni kweli.
Lissu: Hao wote waliosikiliza na wao wameshtakiwa au hawajashtakiwa?
Shahidi: Hilo swali uliuliza, nilishalijibu.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, kuna ambao wameshtakiwa? Shahidi: Hakuna aliyeshtakiwa.
TUHUMA ZAKE
Lissu anakabiliwa na tuhuma za uchochezi na uhaini, akidaiwa kutoa kauli zinazolenga kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Lissu anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo, kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchapisha maneno yafuatayo:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko... kwa hiyo tunaenda kukinukisha sana sana... huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli... tunaenda kukinukisha vibaya sana...”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED