Mikoa nane yafikiwa na mradi vihenge vya kisasa

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 03:47 PM Aug 05 2025
Vihenge vya kisasa vilivyojengwa na TBA
Picha: Pilly Kigome
Vihenge vya kisasa vilivyojengwa na TBA

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA), inakwenda kukamilisha mradi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa (maghala ya kuhifadhia chakula) katika mikoa nane, ili kuleta tija katika sekta ya kilimo nchini.

Mbali na kilimo wakala huo, unatekeleza miradi ya kimkakati katika sekta ya uvuvi na ufugaji, ili kuleta tija kwa makundi hayo na taifa kwa ujumla.

Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa TBA, Renatus Sona, amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya wakulima Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma.

Sona amefafanua mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Ruvuma, Songwe, Njombe, Manyara, Shinyanga na Dodoma.

“Mradi huu utakwenda kuleta tija kwa wakulima na Serikali kwa ujumla kuweza kuhifadhi chakula kisasa na kwenda kuwainua wakulima, kwa kufanya kazi ya kujiamini katika uhifadhi wa chakula nyakati zote pasipo na uharibifu”

Kwa upande wa sekta ya mifugo amefafanua TBA imebuni mradi wa ujenzi wa soko la mnada ya upili mkoani Geita eneo la Mzilayombo, ili wafanyabiashara wa mifugo wauze mifugo yao kisasa.

Amefafanua kwa upande wa sekta ya uvuvi wanaendelea na ujengaji wa mradi wa mabwawa ya kufugia samaki wa maji chumvi katika eneo la Msimbati mkoani Mtwara na Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Mabwawa hayo yataenda kuzalisha vifaranga vya samaki vya maji chumvi na kuongeza tija kwa wafugaji wa samaki, kukua kibiashara ikiwamo kuongeza Pato la Taifa.