Bohari ya Dawa (MSD) imenunua na kusambaza mashine za kisasa zenye teknolojia ya akili mnemba (Artificial Intelligence - AI) kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), zenye thamani ya shilingi milioni 800, ili kuboresha utoaji wa huduma za moyo kwa kiwango cha juu zaidi.
Baadhi ya mashine hizo tayari zimefungwa na zinatarajiwa kuanza kazi muda wowote. Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, ameishukuru MSD kwa hatua hiyo muhimu na kueleza kuwa mashine hizo zitasaidia kupiga picha sahihi kwa ajili ya uchunguzi na kutafsiri taarifa kiautomatiki kwa kutumia AI, hivyo kuongeza ufanisi katika huduma.
Dk. Kisenge pia amepongeza juhudi za MSD katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vya kisasa kwa haraka, hatua inayosaidia taasisi hiyo kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,000, ambapo zaidi ya asilimia 95 hupatiwa huduma kwa kutumia vifaa vya kisasa ikiwemo mashine za ECG na vifaa vya upasuaji wa moyo.
Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Betia Kaema, amesema JKCI ni miongoni mwa hospitali maalum zinazopatiwa huduma kwa haraka na kwa ubora wa hali ya juu, huku MSD ikifanya vikao vya mara kwa mara kuhakikisha mahitaji yao yanatekelezwa kwa wakati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED