Mwandishi wa habari kutoka Kampuni ya Sahara Media Group na mwendeshaji wa kipindi cha The Big Agenda Aloyce Nyanda ametiwa hatiani kwa kosa la kumdhalilisha mitandaoni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ubungo Aron Kagurumjuli.
Baada ya kutiwa hatiani Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Nyanda amemhukumu kumlipa fidia ya Sh.billioni mbili Mkurugenzi aliyedhalilisha katika moja ya machapisho yake mtandaoni.
Akisoma hukumu hiyo ya kesi ya madai ya udhalilishaji namba 6166/202 leo Aprili 11, 2025, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Bonaventure Lema amesema baada ya kusikiliza mpande mbili Nyanda alikutwa na hatia ya kumdhalilisha Mkurugenzi huyo kupitia mitandao yake ya kijamii.
Amesema kosa hilo ni kinyume cha Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kifungu cha 35.
Amesema Nyanda katika mitandao yake ya kijamii alichapisha maudhui ya udhalilishaji dhidi ya Mkurugenzi huyo kwa nyakati tofauti kipindi akiwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na Manispaa ya Kinondoni.
Lema amesema kutokana na hilo mahakama hiyo imemtia hatiani na imemhukumu kulipa faini ya Shilingi bilioni 2, kuomba msamaha kwa yale aliyoyachapisha.
Vilevile imemkataza yeye au mtu yeyote anayehusiana naye kuchapisha taarifa zozote zinamhusu Kagurumujuli ikienda sambamba na kuondoa taarifa alizochapisha kumhusu.
Hata hivyo wakati hukumu hiyo inatolewa si Mshtakiwa wala Wakili wake alikuwepo mahakamani hapo.
Akizungumza nje ya Mahakama wakili wa upande wa Mlalamikaji Erick Mutta amesema ni wakati wa mwandishi huyo kutekeleza hukumu hiyo kwa kuanza kufuta maudhui aliyoyachapisha katika mtandao wake yaliyokuwa ya uongo na yameleta fedhea na kumdhalilisha mtaje wake Aron Kagurumjuli.
"Kwa sasa tunaangalia namna ya utekelezaji wa amri zilizotolewa na mahakama haraka iwezekanavyo kama atashindwa kutekeleza amri hizo zilizotolewa tunaweza kuomba kukamata mali zake," alisema Mutta.
Aidha alisema kama mwandishi huyo hatokuwa na mali za kukamata basi chaguo watakalokuwa nalo ni kumkamata yeye kama mfungwa wa madai.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED