Mwinyi: Tutaongeza nafasi za wenye ulemavu Serikalini

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 02:49 PM Oct 15 2025
Mwinyi: Tutaongeza nafasi za wenye ulemavu Serikalini
PICHA: RAHMA SULEIMAN
Mwinyi: Tutaongeza nafasi za wenye ulemavu Serikalini

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuyazingatia makundi ya watu wenye ulemavu na kuwaongezea nafasi za uteuzi katika awamu ijayo.

Ameeleza kuwa Serikali inalenga kufanya kazi kwa ukaribu na watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwashirikisha kikamilifu kwa kuongeza idadi yao katika nafasi za uongozi na vyombo vya kufanya maamuzi, ikiwemo Baraza la Wawakilishi.

Rais Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa kupitia Sera ya Uwezeshaji, Serikali itaweka mazingatio katika nafasi za uongozi, ajira na elimu kwa watu wenye ulemavu pamoja na kuzingatia mahitaji yao muhimu.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 15 Oktoba 2025, alipokutana na makundi ya watu wenye ulemavu katika mwendelezo wa kampeni zake, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumzia suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi, amesema Serikali itaweka mgao maalum wa fedha kwa ajili ya watu wenye ulemavu pamoja na kutoa mafunzo ili shughuli wanazozifanya ziwe na tija, sambamba na kuongeza mafungu ya fedha kwa ajili ya kuwapatia mikopo.

Kuhusu masuala ya miundombinu, hususan ujenzi wa masoko, Dk. Mwinyi ameahidi kuweka mpango wa kuwapatia maeneo ya kufanyia biashara katika masoko yanayojengwa ili kuinua kipato chao, pamoja na kuhakikisha majengo mapya yanakuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Hata hivyo ameahidi kuondoa ushuru kwa vifaa visaidizi vya watu wenye ulemavu vinavyoingizwa nchini ili kushusha bei ya vifaa hivyo, sambamba na Serikali kuendelea kuwapatia vifaa hivyo bila malipo.