Ndoto za Mpina kugombea urais zagonga mwamba

By Rehema Matowo , Nipashe
Published at 01:08 PM Oct 15 2025
news
Picha Mtandao
Mwanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina

NDOTO za Mwanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, pamoja na chama chake za kuwa na mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, zimegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma kutupilia mbali kesi waliyofungua kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumuondoa mgombea wao kwenye orodha ya wagombea.

Akisoma hukumu yenye kurasa 32 kwa njia ya mtandao, Jaji Frederick Manyanda, akisaidiwa na Majaji Abdallah Gonzi na Sylvester Kainda, amesema kuwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, Mahakama haina mamlaka ya kikatiba kuingilia jambo lolote lililofanywa kwa nia njema na Tume Huru ya Uchaguzi.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 24027 ya mwaka 2025, ilifunguliwa na Mpina kupitia mawakili wake John Seka, Edson Kilatu na Jasper Sabuni, ikipinga uamuzi wa INEC kumuondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Upande wa wajibu maombi uliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Stanley Kalokola, pamoja na Halima Mohamed na Catherine Gwatu kutoka Tume Huru ya Uchaguzi.

Awali, hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Oktoba 10 mwaka huu, lakini iliahirishwa hadi Oktoba 15 kutokana na kutokamilika.

Baada ya uamuzi huo, Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza kupitia taarifa ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa chama kuwa kitakata rufaa, kikisema Mahakama haikusikiliza hoja zake kwa undani.

“Tuliingia kwenye mapambano haya ya kisheria tukiitafuta Haki, Uwazi, na kila mara tumeendelea kusisitiza ushiriki ulio sawa kwenye mchakato wa kidemokrasia ikiwemo Uchaguzi.

“Hata kama Mahakama haikusikiliza maombi yetu kwa muktadha wake (on merit), bado tutaendelea na juhudi za kuitafuta haki na tunu za demokrasia nchini Tanzania,” kimesema cha hicho.

Chama hicho pia kimewapongeza wanachama na wafuasi wake kwa mshikamano waliouonyesha wakati wa shauri hilo, kikitoa wito wa kuendelea kudumisha utulivu na umoja.