WAKATI taifa likiadhimisha kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere leo, bado wosia wake juu ya kupambana na rushwa unabaki kuwa ukumbusho mzito, hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa Uchaguzi Mkuu, ambapo mianya ya rushwa imeendelea kuonekana.
Katika historia ya uongozi wake, Mwalimu Nyerere alisisitiza mara kadhaa kwamba rushwa ni miongoni mwa maadui wakuu wa maendeleo ya taifa, sambamba na ujinga, maradhi na umaskini.
Akizungumza katika moja ya hotuba zake za mwanzo akiwa bungeni, alisema: “Nataka kuongeza adui mwingine katika orodha ya maadui wetu wa umaskini, ujinga na maradhi.
Adui huyu ni rushwa. Rushwa ni adui mkubwa zaidi kwa ustawi wa watu wakati wa amani kuliko hata vita. Inapaswa kushughulikiwa kwa ukatili.”
Katika hotuba yake kwa majaji Machi 15, 1984, Mwalimu Nyerere alikiri kwa uchungu kwamba rushwa na ufisadi vilikuwa tayari vimeanza kuota mizizi katika jamii, akisisitiza kuwa ni dhambi kwa mtu kutendwa upendeleo kwa sababu ya urafiki, cheo au uwezo wa kifedha.
Alitaja umaskini, elimu duni na udhaifu wa mifumo ya utawala bora kama baadhi ya visababishi vya kuenea kwa rushwa, akionya kwamba tabia hiyo ingeweza kuharibu misingi ya taifa. “Huwezi kununua haki,” alisema.
“Haki hainunuliwi. Rushwa yetu siku hizi haina aibu.” Katika hotuba zake za miaka ya 1990, hasa kipindi cha kuelekea uchaguzi wa mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alionya wazi kuhusu rushwa katika siasa.
“Uongozi si biashara, ni utumishi. Mtu anayenunua kura ili achaguliwe, hawezi kuwatumikia watu. Atawatawala kwa kulipiza gharama za kura alizonunua,” alisema Mwalimu Nyerere.
Aliongeza kuwa rushwa kwenye uchaguzi inaua maana halisi ya demokrasia kwa kuwa wananchi hawachagui tena kwa hiari, bali kwa kununuliwa.
“Uchaguzi wa rushwa si uchaguzi, ni biashara. Na nchi haiwezi kuongozwa kwa biashara ya kura,” alisema kwa ukali.
Mwalimu Nyerere pia aliwahi kukemea rushwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema chama hicho kilianzishwa kwa ajili ya wananchi, si kwa ajili ya wenye fedha. “Kiongozi wa kweli ni yule anayechaguliwa kwa sifa, si kwa hongo.
Wananchi, msikubali kuuza kura zenu. Ukimwuzia mtu kura yako, umempa haki ya kukutawala kama mtumwa,” alionya. Ili kuthibitisha uadui wake dhidi ya rushwa, Mwalimu Nyerere aliweka misingi imara ya maadili ya viongozi, akisisitiza kwamba viongozi ni lazima wawe waadilifu, waaminifu na wa mfano katika jamii.
Serikali yake pia iliweka sheria kali dhidi ya rushwa, zikiwamo adhabu za kifungo na hata viboko kwa watakaobainika na makosa hayo.
Zaidi ya miaka 20 baada ya wosia huo, rushwa bado imeendelea kuwa “mfupa mgumu.” Katika mchakato wa sasa wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, vitendo vya rushwa vimeripotiwa kushamiri hasa wakati wa kura za maoni ndani ya vyama vya siasa.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, alikiri hivi karibuni kwamba taasisi hiyo ilipokea taarifa nyingi za vitendo vya rushwa katika hatua za awali za uchaguzi.
“Ni kweli wakati wa mchakato wa kura za maoni tulipokea taarifa nyingi za rushwa, hasa kwa wagombea wanaotafuta kuteuliwa. Tulichukua hatua mbalimbali za kisheria.
Hata hivyo, katika kipindi cha kampeni za vyama, matukio hayo yamepungua kutokana na ufuatiliaji wa karibu,” alisema Chalamila.
Miaka 26 tangu kifo chake, maneno ya Mwalimu Nyerere bado yanabeba uzito uleule kwa taifa linalopambana na rushwa. Alionya mapema kwamba rushwa si tu huiba fedha za umma, bali huiba haki, utu na maadili ya taifa.
“Rushwa ni adui wa haki. Taifa linaloacha rushwa, linajifuta taratibu,” alisema Mwalimu Nyerere. Wakati Tanzania ikiendelea na safari ya uchaguzi mwaka huu, maneno hayo yanabaki kuwa taa ya kuongoza nchi: kukataa hongo, kusimamia haki na kutafuta viongozi wa kweli, si wafanyabiashara wa kura.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED