Serikali imesambaza mashine zaidi ya 100 za kusafisha figo pamoja na vitendanishi vyake katika hospitali mbalimbali nchini, ikiwa ni juhudi za kupunguza gharama za huduma hiyo kwa wananchi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini (CCM), Zacharia Issaay, aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kupunguza gharama za matibabu ya kusafisha figo.
Dk. Mollel alisema serikali imeongeza vituo vya huduma ya kusafisha figo (dialysis) katika hospitali 15 za rufaa za mikoa pamoja na hospitali zote za kanda ili kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo nchini.
Aidha, alisema serikali imeongeza idadi ya wadau na taasisi zinazoingiza vifaa tiba, vitendanishi na dawa, hatua inayolenga kuondoa udhibiti wa soko usio na ushindani na kuhimiza uzalishaji wa ndani kupitia viwanda na ubunifu wa kiteknolojia.
"Serikali imesambaza mashine zaidi ya 100 pamoja na vitendanishi vyake kwenye hospitali za rufaa za mikoa," alisema Dk. Mollel na kusisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote mara utekelezaji utakapoanza, ili kujikinga dhidi ya gharama kubwa za matibabu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED