SIKU YA NYERERE: Mpango alia na rushwa na ufisadi

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 06:01 PM Oct 15 2025
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Ismail Ali Ussi kabla haujazimwa katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya jana.
Picha: Nebart Msokwa
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Ismail Ali Ussi kabla haujazimwa katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya jana.

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ametoa maagizo manne kwa Watanzania kwa ajili ya kuenzi maisha na mchango wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ikiwamo kuimarisha maadili na kulinda tunu za taifa ambazo Mwalimu alizisimamia wakati wa uhai wake.

Akizungumza jana jijini Mbeya wakati wa sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wiki ya Vijana na Maadhimisho ya Miaka 26 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere, Dk. Mpango alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kuenzi urithi wa Mwalimu kwa matendo, si maneno.

"Tukishindwa kuyatekeleza haya kwa vitendo, kuna hatari taifa letu likasambaratika. Kila mmoja wetu anapaswa kusimama katika nafasi yake, ndipo tutakapokuwa tumemuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo," alisema Dk. Mpango.

Agizo la kwanza, Mpango alisema Watanzania wanapaswa kujenga na kuimarisha maadili mema, hasa miongoni mwa vijana na kukemea rushwa na ufisadi ambavyo Mwalimu Nyerere alivichukia kwa maneno na matendo.

Agizo la pili, aliwataka wananchi kulinda uhuru wa taifa, kudumisha umoja, amani na haki, mambo aliyoyataja kuwa nguzo kuu za urithi wa Mwalimu Nyerere.

Agizo la tatu, Makamu wa Rais aliwataka Watanzania wote kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuongeza kipato, kuboresha maisha na kuchangia katika ujenzi wa taifa.

"Hakuna mtu kutoka nje atakayeijenga Tanzania. Ni sisi wenyewe tuna wajibu wa kujenga nchi yetu kwa kufanya kazi kwa juhudi na ubunifu," alisema Dk. Mpango.

Aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa za maendeleo zilizopo kwenye sekta za kilimo biashara, ujasiriamali, teknolojia ya habari (Tehama), huduma, sanaa na michezo, akisema ndizo nguzo muhimu za uchumi wa vijana.

Agizo la nne, alisisitiza umuhimu wa kutunza mazingira, kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti na kudumisha usafi wa mazingira, akisema Mwalimu Nyerere alikuwa mfano wa kuigwa katika mapambano ya uhifadhi wa mazingira.

Awali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema maadhimisho hayo yalitanguliwa na shughuli mbalimbali yakiwamo makongamano zaidi ya 2,000 yaliyofanyika nchi nzima, yakijadili maendeleo ya vijana na falsafa za Mwalimu Nyerere.

"Kwenye vyuo vikuu, kulifanyika midahalo iliyolenga kujadili falsafa za Baba wa Taifa na waasisi wengine wa nchi, huku wanafunzi wakishiriki mashindano ya insha kuhusu historia yake," alisema Majaliwa.

Aliongeza kuwa washindi wa mashindano hayo walipatiwa zawadi, huku vijana wengi wakionesha ubunifu kupitia bidhaa walizozalisha.

Katika kilele cha sherehe hizo, Dk. Mpango aliwakabidhi zawadi wakimbiza Mwenge wa Uhuru waandamizi na halmashauri zilizofanya vizuri katika utekelezaji miradi ya maendeleo.