MWAKILISHI mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchini Tanzania, Dk. Alex Ntale Gasasira, amewasilisha rasmi nyaraka zake za uteuzi, kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Wakati wa hafla hiyo, Dk. Gasasira, alitoa salamu maalum kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, pamoja na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO, Prof. Mohamed Janabi, kwa serikali Tanzania na wananchi wake.
Viongozi hao walieleza pongezi kwa hatua kubwa za maendeleo ambazo Tanzania imepiga, hususan katika sekta ya afya.
“Ni heshima kubwa kwangu kuhudumu nchini Tanzania katika kipindi hiki muhimu kwa afya ya taifa na dunia kwa ujumla,” alisema Dk. Gasasira.
“Shirika la Afya Duniani linabakia mshirika imara wa Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya afya,
kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya, na kuhakikisha kila mtu anafurahia haki yake ya msingi ya kupata huduma bora za afya.”
Chumi, aliishukuru WHO kwa ushirikiano wa muda mrefu na msaada endelevu kwa Serikali ya Tanzania, hasa katika maeneo ya kuimarisha mifumo ya afya, kujenga uwezo wa rasilimali watu, na kuimarisha maandalizi na mwitikio wa dharura za kiafya.
“Serikali ya Tanzania ina dhamira ya dhati kuendeleza ushirikiano wake na Shirika la Afya Duniani kwa lengo la kuboresha afya ya wananchi na kujenga uimara wa taifa katika kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoweza kujitokeza siku zijazo,” alisisitiza Chumi.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa pande zote mbili kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kimkakati, unaoongozwa na ushahidi wa kisayansi, na unaolenga matokeo chanya kwa jamii. Pia, walikubaliana kuhakikisha kuwa shughuli zote za ushirikiano zinaendana na vipaumbele vya afya vya taifa na zinatoa mchango halisi kwa maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na watendaji kutoka Ofisi ya WHO Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED