TEC yabariki Uchaguzi Mkuu, yakemea vitendo vya utekaji,kupotea watu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:28 PM Oct 14 2025
TEC yabariki Uchaguzi Mkuu, yakemea vitendo vya utekaji,kupotea watu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limebariki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, likiwataka Watanzania kushiriki kwa amani, umoja na kwa kuongozwa na dhamiri safi, huku likikemea vikali matukio ya utekaji na kupotea kwa watu yanayoripotiwa katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, Oktoba 14, 2025, na Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Amani ya TEC, Askofu Juda Ruwa’ichi, wakati wa Maadhimisho ya Umoja wa Wanaume Wakatoliki Tanzania.

Askofu Ruwa’ichi amesema kuwa uchaguzi ni tukio muhimu la kikatiba, ambapo wananchi wanatumia haki yao kuwapa viongozi dhamana ya kuongoza nchi, hivyo ni lazima kufanyika kwa amani, haki na uwazi.

“Uchaguzi Mkuu ni tukio la kikatiba kwani hapo ndipo wananchi hutegemewa kuwapa waliowachagua dhamana ya kutawala na kuongoza nchi,” amesema.

Ameongeza kuwa, wakati Tanzania ikiendelea kumkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni muhimu pia kutafakari historia ya nchi na misingi ya haki, umoja na demokrasia aliyoiweka katika masuala ya uchaguzi.

“Tanzania inapomkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni vema kutafakari kuhusu nchi na historia yake katika masuala ya Uchaguzi Mkuu,” ameongeza.

Aidha, Askofu Ruwa’ichi amewataka wananchi wote kuelekea uchaguzi huu kuongozwa na dhamiri safi, yenye hofu ya Mungu, na wasikubali kurubuniwa kwa vitisho au ahadi za muda mfupi.

TEC imesisitiza kwamba amani, heshima ya utu na haki za binadamu ndizo nguzo kuu za uchaguzi huru na wa haki, na kuwataka wadau wote wa kisiasa kuhakikisha kampeni na zoezi la uchaguzi linafanyika bila uvunjifu wa amani.