Vijana wahimizwa kuweka akiba kuendeleza uzalendo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:51 PM Oct 14 2025
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said

KATIBU Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, amewataka vijana nchini kujiwekea utamaduni wa kuweka akiba kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii, ili kujihakikishia usalama wa kifedha na ustawi wa maisha yao ya baadaye.

Amesema hatua hiyo itawawezesha vijana kupata huduma muhimu kama mikopo, matibabu, mafao ya uzeeni na fursa nyingine za kiuchumi zinazotolewa na mifuko hiyo.

Mhandisi Zena amebainisha hayo Oktoba 13, 2025 wakati akifunga Kongamano la Siku mbili la Vijana, jijini Mbeya.

Vijana wahimizwa kuweka akiba kuendeleza uzalendo
Aidha, amesema vijana ndio nguvu kazi ya taifa, hivyo ni muhimu kuwekeza katika mustakabali wao kwa kupanga matumizi yao na kujiunga na mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii. 

“Kijana mwenye utamaduni wa kuweka akiba ni kijana mwenye dira ya mafanikio, anayejali kesho yake na anayechangia katika maendeleo ya taifa,” amesema.

Aidha, amewahimiza vijana kudumisha uzalendo, kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani na kujiepusha na makundi yanayopandikiza chuki au misimamo mikali.