Kampeni za Chama cha NCCR-Mageuzi zimeendelea kwa kasi jijini Mwanza, ambapo viongozi wa juu wa chama hicho wamehimiza wananchi kudumisha amani na kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Ilemela, Mgombea Mwenza wa Urais, Dk. Eveline Munisi, alisisitiza umuhimu wa kulinda amani, akibainisha kuwa Tanzania imekuwa mfano wa utulivu na kimbilio kwa mataifa jirani yanayokumbwa na migogoro.
“Tanzania ni nchi ya amani, na amani hii ndiyo msingi wa maendeleo yetu. Tukiiweka rehani, tutakuwa tumepoteza kila kitu kwa sababu hatuna pa kukimbilia,” alisema Dk. Munisi.
Kwa upande wake, Mgombea Urais wa NCCR-Mageuzi, Ambary Haji Khamis, aliwataka Watanzania wote kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, akisisitiza kuwa kushiriki katika uchaguzi ni haki na wajibu wa kikatiba.
“Uchaguzi ni sauti ya wananchi. Kila kura ina thamani kubwa katika kuamua mustakabali wa nchi yetu. Nawasihi msikose kushiriki,” alisema Khamis.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED