BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), limesema watu wanaojinasibu kwamba wanamudu kuwawezesha wananchi kiuchumi na kumbe ni udanganyifu, wanakiuka Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Sura 386.
Mwanasheria wa NEEC, Emmanuel Kalengela, amesema hayo, mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam, akitoa elimu kuhusu uwezeshaji kiuchumi wananchi.
"Sheria yetu ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi imeanza mwaka 2004 lakini tumekuwa na mabadiliko ambayo yamefanyika hivi karibuni mwaka 2025 na kupitishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mwezi wa tatu.
"Katika kuhakikisha kwamba suala la uwezeshaji linafanyika vizuri lakini pia hakuna upotoshaji. Hakuna mtu ambaye anamdhulumu sheria yetu imeweka mazingira mazuri,” amesema.
Amesema watu wanaotoa matangazo kwenye mitandao kwa wanawawezesha wananchi wengi wao, ni waongo na kuwaibia wanajamii.
"Sheria inakuja na kudhibiti kitu kama hicho kwa kuweka adhabu ya kifungo mwaka mmoja pamoja na faini isyopungua 500,000 na isiyozidi Sh. milioni 50,” amesema Kalengela.
Awali, Kaimu Katibu Mtendaji NEEC, Neema Mwakatobe, amesema jamii inapaswa kupata fursa sawa za kiuchumi, ili kupata mafanikio kwa manufaa yao na taifa.
Amesema baraza hilo, linatoa mafunzo kwa waandishi wa habari, ili kuwajengea, hatua inayolenga kuhakikisha taarifa sahihi za uwezeshaji zinawafikia wananchi kote nchini.
“Wananchi hawawezi kuwezeshwa kiuchumi bila taarifa sahihi. Kupitia nyinyi, wananchi wataweza kujua wapi pa kupata msaada wanapokutana na changamoto za kiuchumi, wanavyoweza kushiriki shughuli za maendeleo,” amesema Mwakatobe.
Amebainisha kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025, NEEC imetumia Sh. trilioni 2.44 kutoa mikopo kwa wanufaika wapatao milioni 18, wanaume wakiwa asilimia 51 na wanawake asilimia 49.
Amesema fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa NEEC, Gwakisa Bapala, amesema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 10 pekee ya watanzania, waliokuwa wananufaika moja kwa moja na ukuaji wa uchumi kutokana na changamoto za mitaji, ujuzi, masoko na miundombinu duni.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (JOWUTA), Selemani Msuya, amesema elimu hiyo ni muhimu, akisema waandishi inawajengea uwezo wa kuzibaini changamoto kwenye jamii na kuzianisha na kupatiwa ufumbuzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED