Wanafunzi wawafariji wenzao wanaotoka mazingira magumu

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 06:12 PM Oct 15 2025
Zawadi mbalimbali zilizotolewa na wanafunzi wa sekondari ya Rwepa’s kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha New Hope.
PICHA: SHABAN NJIA
Zawadi mbalimbali zilizotolewa na wanafunzi wa sekondari ya Rwepa’s kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha New Hope.

WANAFUNZI wa Shekondari ya Rwepa’s iliyopo kata ya Mhungula Manispaa ya Kahama, wamewatembelea wanafunzi wenzao wanaotoka mazingira magumu na kuwataka kuacha kujinyanyapaa na badala take wajikite katika elimu ili kutimiza ndoto zao.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika sekondari hiyo, Dorce Fulgency ameyasema haya leo wakati walipowatembelea watoto wanaolelewa katika kituo cha New Hope kilichopo Mwime Ilindi na kusema, akimaliza masomo na kupata kazi atawashika mkono watoto wanaotoka mazingira magumu nchini.

Amesema, hali ya kuwa yatima, kutelekezwa au kunyanyapaliwa haipaswi kuwa kikwazo cha mafanikio kielimu hivyo wasome kwa bidii na kuhakikisha kila mmoja anatimiza malengo yake ili hapo baadae aje kuwa msaada mkubwa kwenye makundi hayo.

 Nae Rehema Malima mwanafunzi wa kidato cha tatu amesisitiza kuwa ndoto za kuwa madaktari, walimu, wahandisi na viongozi wa kesho hazizuiliki na hali ya sasa ya mazingira waliyopo imradi tu kuna nia na bidi katika masomo.

 Mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo Joseph Sospeter amesema, wamejifunza kuwa maisha ni changamoto lakini si mwisho wa ndoto zao na kusoma kwa bidii ndiko kutakakoleta mabadiliko katika maisha yao na kuwaomba wadau kujitokeza na kuwasaidia mahitaji ya shule ambayo ndio hitaji lao kubwa kielimu.

 “Wengi hudhani yatima hawawezi kufaulu, sisi tunasema tunaweza na tutafaulu tumekuwa tukihimiza ili tusiogope maisha bali tuyakimbilie kwa maarifa na nidhamu”Amesema

 Mkurugenzi wa sekondari ya Rwepa’s Frank Samweli amewaunga mkono wanafunzi kwa kutoa mahitaji mbalimbali kama vile, sabuni za kufulia na kuogea, peni na pensel, mchele kg 70, soda na mafuta ya kula lita 20 na kuwataka wengine kujitoa kusaidia Kundi hilo.

 Mmiliki wa kituo hicho, Suleiman Juma amewapongeza wanafunzi hao kwa kuwatembelea wenzao na kuwafariji kwa mahitaji mbalimbali na kuwapati imani ya kuendelea kufanya vema kwenye masomo yao ili wasijinyanyapae na kutimiza malengo yao kielimu.

 Amesema, watoto hao wamekuwa na mabadiliko makubwa ya kifikra na kitaaluma kutokana na mafunzo ya mara kwa mara kuhusu thamani ya elimu na wapo waliofanya vema kwenye mitihani ya darasa la saba na kujiunga na sekondari na wanaamini kuwa elimu ndio urithi bora kwao.