Watu 345 waliopima mkesha wa Mwenge wakutwa na VVU

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 06:06 PM Oct 15 2025
Riboni nyekundu alama inayotumika kulinda utu
Picha: Mtsndao
Riboni nyekundu alama inayotumika kulinda utu

WATU 345 kati ya 62,257 waliojitokeza kupima afya zao kwa hiari katika mikesha ya Mwenge wa Uhuru kwenye halmashauri mbalimbali nchini, wamebainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), hali inayoonyesha kwamba changamoto ya ugonjwa huo bado ni kubwa.

Takwimu hizo zilitolewa jana jijini Mbeya na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, wakati wa sherehe za kitaifa za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wiki ya Vijana na Maadhimisho ya Miaka 26 ya Kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Ridhiwani alisema idadi hiyo ya watu waliobainika na maambukizi inawakilisha asilimia 0.6 ya wote waliojitokeza kupima, na kwamba wote walipatiwa ushauri nasaha na kusajiliwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kuanza matibabu.

"Lakini pia, katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, watu 28,228 walijitokeza kupima na kati yao, 831 sawa na asilimia 3.1 walibainika kuwa na maambukizi ya vimelea vya ugonjwa huo. Wote walipatiwa matibabu," alisema Ridhiwani.

Aidha, waziri huyo alisema Mwenge wa Uhuru mwaka huu ulikimbizwa zaidi ya kilomita 25,000 na kutembelea miradi 1,382 yenye thamani ya zaidi ya Sh. trilioni 2.9, ikiwamo miradi iliyotekelezwa kwa fedha za ndani za halmashauri.

Akisoma risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ismail Ali Ussi, alisema hakuna mradi uliokataliwa mwaka huu, hatua inayoonesha ongezeko la uwajibikaji na ubora wa utekelezaji miradi nchini.

"Baadhi ya miradi tuliyokagua ilikuwa na kasoro ndogo ndogo za kiufundi, lakini tulielekeza zifanyiwe marekebisho na taarifa za utekelezaji ziwasilishwe kwenye wizara husika," alisema Ussi.

Aliongeza kuwa baadhi ya taasisi za serikali zimekuwa zikipinga miradi yao kutembelewa na Mwenge wa Uhuru, kwa madai kwamba miradi hiyo inapaswa kutembelewa na viongozi wa juu wa nchi, jambo alilolielezea kuwa linapaswa kuangaliwa upya.

"Tunashauri serikali ielekeze taasisi zote kuruhusu miradi yao kutembelewa na Mwenge wa Uhuru, kwani ni fursa muhimu ya ukaguzi, uwazi na uwajibikaji," alisema Ussi.

Alipendekeza pia kila mkoa nchini uwe na vifaa vya kisasa vya kupima ubora wa barabara ili miradi ya miundombinu itekelezwe kwa viwango vinavyokubalika.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, aliomba serikali kuharakisha utekelezaji miradi mikubwa ya maendeleo mkoani humo, ukiwamo Mradi wa Maji wa Chanzo cha Mto Kiwira na upanuzi wa barabara ya TANZAM (Tanzania–Zambia Highway).

Mwenge wa Uhuru ulihitimisha mbio zake jana jijini Mbeya, na unatarajiwa kuwashwa tena mwaka ujao katika Mkoa wa Kusini Pemba na kuzimwa katika Mkoa wa Rukwa.