Waziri ulega akutana na kijana mwenye kipaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:55 PM Jul 20 2025
news
Picha Mtandao
Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega akimuonyesha kijana mwenye kimaji moja ya eneo alilotamani kuliona.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amekutana na kuzungumza na kijana mwenye kipaji cha usanifu wa madaraja, ambako amemtembeza katika maeneo mbalimbali ili kujionea maeneo aliyotamani kufika ndani ya mkoa wa Dar es Salaam.

Siku chache zilizopita, kulisambaa picha mjongeo za kijana huyo Ridhiwani Asheri (13) kwenye mitandao ya kijamii zikiionyesha uwezo wake wa kubuni ujenzi wa barabara na madaraja akiwa kijijini kwao Kibaigwa, Dodoma. 

Baada ya Waziri Ulega mwenye dhamana ya masuala ya ujenzi nchini kuona picha hizo, aliagiza wataalamu wa wizara yake kwenda kumwona na kuangalia namna ya kumsaidia. 

Baada ya kumwona na kuzungumza na familia, waziri aliomba mkutano nao ili kuangalia namna bora ambayo serikali inaweza kufanikisha ndoto zake. 

Baada ya kukutana na familia yake leo Dar es Salaam, Ulega amesema "serikali ya Tanzania ina historia, uwezo na dhamira ya kusaidia watoto wenye uwezo mkubwa kimaarifa kwa maslahi ya taifa". 

1
Pia Waziri Ulega ameahidi kumsaidia kijana huyo kuhakikisha anatimiza ndoto zake za kuwa mhandisi mkubwa hapo baadaye.

Waziri Ulega amesema atakaa na Wizara ya Elimu kuona ni sehemu gani sahihi kijana huyo apelekwe ili kuweza kumsaidia kielimu hasa kwenye maswala ya ujenzi.

Miongoni mwa maeneo kijana hiyo aliyotamani kuyaona na kupelekwa na waziri huyo ni Daraja la Kijazi lililopo Ubungo, Daraja la Tanzanite na kituo cha Treni ya Mwendokasi (SGR) Posta.