KWA DAKIKA 11; Historia wanawake sita wazuru anga za mbali

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:15 PM Apr 15 2025
Roketi
Picha: Mtandao
Roketi

NI tukio la kihistoria lililotikisa dunia, roketi ya New Shepard, inayomilikiwa na kampuni ya Blue Origin ya Jeff Bezos, ilirushwa kutoka Texas, Marekani, ikiwa imebeba wanawake sita, waliounda kundi la kwanza la wanawake pekee kufika angani tangu mwaka 1963.

Kwa mara ya kwanza katika miaka zaidi ya 60, wanawake pekee wanasafiri kwenda anga za mbali bila kujumuika na mwanaume.

Safari hiyo ya kihistoria ilidumu kwa dakika 11 pekee, lakini ilibeba maana kubwa zaidi ya muda huo mfupi. 

Wanawake hao walivuka mpaka wa anga, unaotambulika kimataifa mstari wa ‘Kármán’ na kurudi salama duniani’ huku wakiweka alama ya milele katika historia ya safari za anga.

Roketi
Mwanamuziki Katy Perry, alijiunga na mpenzi wa mfanyabiashara Jeff Bezos, Lauren Sanchez, mtangazaji wa televisheni ya CBS Gale King, mwanasayansi wa makombora wa NASA Aisha Bowe, mwanaharakati wa haki za binadamu Amanda Inguen, na mtayarishaji wa filamu Garrett Flynn.

Roketi ilirushwa kwa kasi na ndani ya dakika saba, chombo cha anga kilitenganishwa na roketi na kutupwa angani kama jiwe linavyotupwa juu, chombo hicho kikavuka mpaka wa anga na kuwapa wanawake hao hisia ya kutokuwa na uzito wakiwa juu ya mstari wa Kármán, takribani kilomita 100 kutoka usawa wa bahari.

Chombo hicho kilikuwa kinajiendesha chenyewe, kisichohitaji rubani wala uendeshaji kutoka kwa abiria. 

Baada ya muda mfupi wa kuangalia uzuri wa dunia kutoka juu na kupata uzoefu wa na hisia za kipekee kama kundi la wanawake walioandika historia, chombo kilianza safari ya kurudi duniani.

Blue Origin, imefanya safari nyingi kama hii lakini hii ilikuwa maalum. 

Lengo la Safari hii ilikuwa ni kuhamasisha utalii wa anga. 

Na wenyewe wanasema lengo si tu kukuza sekta ya utalii wa anga, bali pia kuvunjilia mbali mitazamo ya kijinsia, kuonesha kuwa wanawake nao wana nafasi katika maeneo ya juu kabisa ya mafanikio ya kibinadamu, ikiwemo hili la kusafiri anga za mbali, linaloonekana haliwezekani bila mwanaume

Kama ilivyoelezwa na Blue Origin: "Hii si misheni ya kawaida ya anga. Ni misheni ya kuhamasisha vizazi vijavyo."

Chombo kilitua taratibu kwa msaada wa parachuti katika jangwa la Texas. 

Wakati huo huo, chombo kilichokuwa kinaendesha roketi kilichokuwa kimewatuma huko angani, kilitua chenyewe umbali wa kilomita chache kutoka eneo ambalo walianza safari.

Baada ya kutua, bilionea Jeff Bezos, mwenyewe alikuwapo kuwakaribisha. 

Katy Perry na Gayle King, waliibusu ardhi kwa furaha walipotoka kwenye chombo hicho, ishara ya kushukuru maisha na mafanikio hayo.

Wakati wa uzinduzi na kuanza kwa safari, familia na marafiki walikuwapo, akiwamo Oprah Winfrey, baadhi ya familia ya Kardashians na kundi la wanawake wana anga. 

Machozi ya furaha yaliwatiririka wote walipoona chombo kimetua salama kutoka anga za mbali.

Kila mmoja wa wanawake hao alitoa maneno ya kugusa moyo, baada ya tukio hilo na kutua salama duniani:

Gayle King: "Nilihitaji tu kuchukua muda na kuthamini ardhi."

Lauren Sánchez: "Kulikuwa na mshikamano wa ajabu kati yetu. Najivunia sana kikosi hiki."

Amanda Nguyen: "Nilijiapia kamwe sitakata tamaa. Leo nashukuru kwa safari hii ya kipekee."

Kerianne Flynn: "Rafiki wa mwanangu alimwambia 'Mama hawaendi angani'. Lakini mama huyu ameenda angani!"

Aisha Bowe: "Sitakuwa mtu yule yule tena. Kulikuwa na nishati ya kipekee ndani ya kapsuli."

Katy Perry: "Kwenda angani ni jambo la pili kwa umuhimu baada ya kuwa mama. Labda nitapiga wimbo kuhusu hili!"

MSTARI WA KÁRMÁN NI UPI

Mstari wa Kármán, ni mpaka wa kufikirika unaotambulika kimataifa kuwa ndio mwanzo wa anga ya juu na dunia, kilomita 100 kutoka usawa wa bahari.

Kulingana na Fédération Aéronautique Internationale, eneo hili linatenganisha anga ya Dunia na anga ya nje (astronomia).

 Kwa mujibu wa Profesa T.V. Venkateswaran, asilimia 99.9 ya anga ya dunia ipo chini ya mstari huo, hivyo yeyote anayevuka mstari huo anachukuliwa kama msafiri wa anga za mbali.

BBC